Wednesday, September 19, 2012

Wizara Ya Nishati Na Madini Yatoa Maagizo



 
Naibu waziri wa Nishati na Madini Mhe. Stephen Masele akitoa maagizo alipotembelea ofisi za TMAA, kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa TMAA, Bw. Paul Masanja.


Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya madini, Stephen Masele ameiagiza Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) kuimarisha ukaguzi maeneo ya migodini hususan maeneo ya migodi mikubwa.

Mhe.Maselle alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za Wakala zilizopo maeneo ya Kurasini jijini Dar es Salaam.
Alibainisha kuwa TMAA haina wakaguzi ambao wanakuwa ndani ya mashimo ya migodi hiyo hivyo kuna umuhimu wa kuwa na mkaguzi mwingine ambaye atakuwa maalumu kwa ajili ya kufanya ukaguzi ndani ya mashimo.

“Ugakuzi makini utahusika pia na kuhakiki gharama za uwekezaji na uendeshaji wa migodi mikubwa ya ili kudhibiti mapato ya Serikali”, alisema Masele na kuongeza kuwa madini yanayosafirishwa kwa mashine kutoka katika mashimo ni kiasi kidogo tofauti na yale ambayo yanatolewa kwa kuokotwa kwa mkono kutoka huko katika mashimo.

Aidha, Naibu Waziri huyo aliipongeza TMAA kwa kufanikisha kukamatwa kwa mameneja watatu wa Kampuni ya Aureus Ltd ambao wanatuhumiwa kukwepa kodi na kutorosha dhahabu nje ya nchi. “TMAA ni jicho la Wizara, mmefanya ukaguzi na mmebaini haya, endeleeni hivyo hivyo, taarifa zote mtakazoleta tutazifanyia kazi”, alisisitiza.
Alisema ukaguzi uliofanywa na TMAA unaonesha uzalishaji wa kampuni hiyo ni mkubwa kuliko uliokuwepo kabla ya kuanza kwa ukaguzi. “Tukigundua vitendo vya utoroshaji ama ukwepaji wa kulipa mapato kwa namna yoyote, tutachukua hatua kali ili iwe ni fundisho kwa wengine wenye tabia za namna hii” alionya.

Naye Mtendaji Mkuu wa TMAA, Paul Masanja alisema TMAA itaendelea kufanya kazi kwa kasi zaidi ili kuendelea kuwabaini wale wote wasiyowaaminifu na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake.
 
“Tunakuahidi Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba sisi hatutorudi nyuma, tutaendelea kutoa ushirikiano wa karibu zaidi na tutafanya kazi zetu kwa ufanisi ili kufikia malengo” aliongeza.