Tuesday, September 18, 2012

WANANCHI ILEJE WATAKIWA KUWA MAKINI


 
Mkuu wa Wilaya ya Ileje, RoseMary Senyamule   

 


WANANCHI wametakiwa kuwa makini na watu wanaowambia maneno ya upotoshaji juu ya uchangiaji wa maoni ya uundwaji wa katiba mpya badala yake wawe na tabia ya kujitokeza wao wenyewe kwenye mikutano hiyo.

Imeelezwa kuwa wananchi wengi wamekuwa wavivu kuhudhuria mikutano yenye lengo la kuleta maendeleo badala yake wanakaa kusikiliza maneno ya uzushi na kukimbilia kuilaumu serikali.


Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Ileje, RoseMary Senyamule  wakati wa mdahalo wa kuwandaa na kuwahamasisha wananchi kuhusu utoaji maoni ya katiba, ambapo alisema kuwa upatiakanaji wa katiba mpya yenye kukidhi mahitaji ya wananchi unategemea mawazo wanananchi wenyewe.

Mdahalo huo uliandaliwa na mtandao wa mashirika yasio ya kiserikali wilayani Ileje kwa ufadhili wa shirika la the Foundation Civil Society uliokuwa na lengo la kuwatayarisha wananchi kabla ya tume ya kukusanya maoni kufika wilayani humo.


Alisema kuwa mahudhurio ya wananchi katika mikutano ya kutoa maoni ndio yanaweza kusadia upatakanaji wa katiba nzuri yenye mawazo shirikishi kutoka kwa makundi mbalimbali ya jamii ambayo yatapewa nafasi ya kutosha kuchangia mawazo na maoni yao kuhusu katiba mpya.

"itasikitisha kama wananchi watashindwa kufika na kushiriki katika mikutano ya tume ya kukusanya maoni ya katiba, maana hii ni fursa pekee kwa wale ambao tume hiyo itapita karibu na maeneo yao, na kama wananchi watashindwa kufanya hivyo badaye wasilaumu kwa yale yote yatakayo kuwa yemingizwa katika katiba" alisema.

Aliongeza kuwa Wilaya ya Ileje ni miongoni mwa wilaya ambayo ipo mpakani mwa nchi ambapo alisisitiza wananchi wasisite kuingiza maoni kuhusu hali ya mipaka ya nchi yao katika katiba itakayo andaliwa.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliohudhuria mdahalo huo walisema maandalio ya katiba mpya yazingatie mahitaji ya makundi maalumu na jinsia pamoja haki ya wananchi kumiliki ardhi yao ili kuondoa migogoro kati yao na wawekezaji, na kwamba kwa sasa watanzania hawana haki juu ya ardhi yao kutokana na wawekezaji kupewa nafasi zaidi kuliko wazawa.

Pia walisema suala la wanawake kunyang'anywa mali na ndugu wa waume zao mara baada ya kufariki ni kukiuka haki pia ni unyanyasaji wa kijisia dhidi ya watoto wa marehemu na mke kwa kuwa mke alishiriki kikamilifu katika utafutaji wa mali hizohivyo suala hilo litambuliwe kikatiba.