Sunday, September 23, 2012

WAKAZI SINGIDA WALALAMIKIA MAVAZI YA WANAFUNZI WA KIKE WA VYUO VYA UHAZILI NA UHASIBU.



Mkuu wa wilaya ya Singida Mwalimu Queen Mlozi akizungumza na wananchi wa kata ya Utemini manispaa ya Singida ahamasisha maadili mema kwa watoto.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu
Baadhi ya ya wakazi wa manispaa ya Singida wamelalamikia mavazi yanayovaliwa na wanafunzi wa vyuo vya uhazili na uhasibu, kwa madai kwamba yanachangia kuharibu maadili ya watoto wao.
Malalamiko hayo yametolewa na wakazi  hao kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Utemini mjini Singida katika mkutano ulioitishwa kwa ajili ya mkuu wa wilaya ya Singida, Mwalimu Queen Mlozi kuhamasisha ujenzi wa maabara katika shule za sekondari za kata.
Wakifafanua, wamesema wanafunzi wa vyuo hivyo na hsasa wa kike, wanavaa nguo ambazo ni kinyume na maadili ya kitanzania na zinachochea vitendo vya ngono zembe.
“Mheshimiwa mkuu wa wilaya, nguo zinazovaliwa na hawa wanafunzi wa kike, zinaacha nusu ya mwili ubaki kama alivyozaliwa na mbaya zaidi zinawabana kupindukia, na Kwa upande wa wanafunzi wa kiume, wao suruali zao wanazivaa chini kabisa ya makalio” almeema Ntandu Jumbe.
Wamesema uvaaji wa nguo unaofanywa na wanafunzi wa vyuo hivyo, unachochea kasi ya mmomonyoko wa maadili kwa vijana na atoto wao kuongezeka mara dufu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Queen Mlozi amesema tatizo hilo na yeye amelibaini lakini hata hivyo, akadai kuwa hayo ni matunda ya utandawazi.
Amesema tatizo la kuharibika kwa watoto kwa maana ya kutokuwa na maadili mema ni la karibu kila familia na hivi sasa ni kubwa mno.
Queen Mlozi amesema kwa kweli dawa pekee hivi sasa ya kupambana na janga hili la watoto kuharibika, ni sisi sote wazazi, walezi, viongozi wa serikali na wa madhehebu ya dini, kuunganisha nguvu zetu pamoja na kuimba wimbo mmoja, nao ni wa malezi bora kwa watoto wetu.
Aidha, mkuu huyo wa wilaya ameagiza kwamba kuanzia sasa kila vikao vya maamuzi vya ngazi mbalimbali, ajenda yao kuu iwe ni mkakati wa kudhibiti kasi ya mmomonyoko wa maadili kwa watoto.