Friday, September 21, 2012

TAARIFA YA UONGOZI WA HOTEL YA PETER SAFARI’s KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSIANA NA MADAI YALIYOTOLEWA NA KOCHA WA TIMU YA YANGA BAADA YA KUMALIZIKA MCHEZO WAKE NA TANZANIA PRISON TAREHE SEPT 15, 2012.



KOCHA WA YANGA TOM SAINTFIET 


Ndugu wanahabari,

Karibuni katika mkutano mfupi ambao unalenga kuzungumzia  ama kuelezea masikitiko makubwa dhidi ya Kocha wa Timu ya Yanga TOM SAINTFIET aliyoyatoa kwa vyombo vya habari kuidhalilisha hoteli  yangu   juu ya huduma zake na kiwango chake alichokiita cha huduma 
mbovu!.

Kimsingi management ya  Peter safari’s Hotel na Uongozi wa chama cha wamiliki wa Mahotel Mkoa wa Mbeya, tumesoma na kusikiliza kwa masikitiko makubwa lawama zilizotolewa na Kocha huyo kuwa “hajawahi kulala kwenye hoteli ya hadhi ya chini kama hii  katika nchi 20 alizowahi kufanya kazi katika nchi za Afrika”.

Uongozi wa hotel  na chama cha wamiliki wa hotel kwa ujumla kinachukulia suala hili kama kampeni maalumu ya kudhalilisha na kukatisha tamaa wateja kuiona mbeya haina hotel za hadhi za kuishi timu na watu wenye hadhi katika jamii, kitu ambacho si kweli na ni visingizio kutokana kushindwa kwake kuwezesha timu kufikia matarajio  ya mashabiki na wapenzi wa timu hiyo.

Kimsingi viongozi wa Timu ya yanga waliomba kuwalaza wachezaji wawili katika kitanda kimoja tofauti na taratibu za hotel na hii ilitokana na mipangilio yao hasa kwenye suala la uwezo wa kulipia kila mchezaji chumba chake, aidha, uongozi wa hotel ulijitahidi kwa kadri ya uwezo wake kuhakikisha kuwa wachezaji wanapata huduma walizohitaji na hata wakati mwingine kutoa usafiri kwaajili ya kununua mahitaji ya familia zao kitu ambacho hakifanyiki maeneo mengine kwa gharama za hotel.

Kwa kutambua madhara yaliyotokana na matamshi ya kocha huyo raia wa Ubelgiji, Uongozi wa hotel ya Peter Safaris  unayaona matamshi haya kama udhalilishaji mkubwa  na wenye nia mbaya ya kuuharibia mkoa wa mbeya  na kuutangaza vibaya kwa wageni  juu ya uwezo wake katika utoaji wa  huduma za hoteli.

Aidha  kwakuwa maneno ya kocha huyo  yametamkwa na kutangazwa kwenye vyombo vya habari pasipo kukanushwa na viongozi wa Timu ya Yanga ambao ndiyo waliofanya maandalizi na kufanya mazungumzo ya maombi  ya kuwalaza wachezaji wawili katika vyumba ambavyo vina uwezo wa kulaza mtu mmoja (single), Peter safaris inaliona jambo hilo kama ni sehemu ya kashfa iliyojengwa kwa nia ya kuiharibia hotel biashara  na kuipotezea hadhi mbele ya wageni  na watumiaji wa huduma za PETER SAFARIS  ambayo inaendelea kupanua huduma zake kwa mkoa wa mbeya na maeneo mengine.

Ikumbukwe kuwa Peter safaris hotels imekuwa ikipokea wageni wa hadhi mbalimbali wakiwemo viongozi wa ngazi za kitaifa, wageni kutoka nje wa hadhi za juu na wafanyabiashara wakubwa, hivyo ugeni wa Yanga na hadhi inayozungumzwa na Kocha huyo hauwezi kufikia mahala pa kuidhalilisha hotel kwa kiwango hicho ambacho kocha huyo amevitumia vyombo vya habari licha ya hotel kutopata maoni yoyote baada ya timu  kuhudumiwa   kwenye sanduku la maoni(suggestion box).

Kutokana na hali hii iliyojitokeza, uongozi wa Hotel unautaka uongozi wa Yanga kuiomba radhi management ya Hotel ya Peter safaris kwa lugha ya kashfa na isiyoendana na utamaduni wa Mtanzania kwakuzingatia kuwa wachezaji wakiulizwa namna walivyohudumiwa wasingeweza kuzungumza hayo ambayo mwalimu wao ameyazungumza kwa utashi wake.

PETER SAFAR’s inalichukulia jambo hili kwa uzito unaostahili kwakuzingatia kuwa  lugha iliyotolewa na mteja wake huyo imevuka kiwango cha kuvumilika, na njia pekee ambayo tunadhani ni ya uungwana kabla ya kuingia kwenye taratibu za kisheria ni kuwataka YANGA kuomba radhi kwa lugha ya dharau na kashfa dhidi ya hotel yetu vinginevyo tunakusudia kuchua hatua za kisheria kwa kuzingatia kuwa hotel inaendeleshwa kwa mujibu wa taratibu na sheria zinazotawala huduma za hotel na zile za mipango miji
 ambazo masuala ya usafi ni miongoni mwa maeneo muhimu ya kukidhi viwango vya uendeshaji wake.
Ninawashukuruni kwa  mahudhulio yenu


Nawasilisha
MKURUGENZI  MTENDAJI
PETER SAFARI’s HOTEL
MBEYA.  
20/09/2012