MRATIBU wa Ukimwi katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Exavery Kehegwa na aliyekuwa Mhasibu wa Manispaa hiyo, Christina Nyamahinzu wamepandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Kigoma na kusomewa mashitaka mawili ya kula njama za kuiibia Serikali na kumdanganya mwajiri.
Mbele ya Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo, David Ngunyale Mwendesha Mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Moses Malewo alisema kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo wakati wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Ilielezwa mahakamani hapo kwamba watuhumiwa wanadaiwa kuandika taarifa wakieleza kuwa Oktoba 9 mwaka 2010 waliandaa semina ya siku mbili ya Ukimwi kwa wadau 22 wa manispaa hiyo huku kila mjumbe akilipwa Sh 20,000 kwa siku wakati si kweli.
Kwa mujibu wa Mwendesha Mashitaka huyo kutoka Takukuru, watuhumiwa wanadaiwa kufanya kosa hilo kinyume na kifungu namba 22 cha sheria ya makosa ya adhabu.
Watuhumiwa wote walikana makosa yao na kwamba kesi hiyo itaitwa tena mahakamani hapo Oktoba 9 mwaka huu ambapo hoja za awali kwa watuhumiwa zitawasilishwa.