Saturday, September 22, 2012

GAZETI LA DIRA YA MTANZANIA LAAMRIWA KUMUOMBA RADHI WAZIRI MKUU MSTAAFU EDWARD LOWASSA MARA MOJA



Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa akisaini hati mbele ya kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT)

---- 

Kamati ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeeleza kuwa Gazeti la Dira  ya Mtanzanianewspaper limedhalilisha  taaluma ya uandishi wa habari kwa  kuchapisha taarifa za kashfa dhidi ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa bila kumpa nafasi ya kujibu.

Akitangaza  uamuzi wa kamati hiyo iliyoketi Jijini Dare s Salaam Septemba 20,2012,  Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jaji Thomas Mihayo alisema madai yaliyochapishwa na gazeti hilo  yanaudhi, yanadhalilisha na yanaleta dharau.Vile vile taarifa ya  gazeti hilo ya madai kuhusu Rais Kikwete ni ya hatari na sawa na uhaini, alisema Jaji MihayoJaji huyo pia alisema kuwa  gazeti hilo pia limeivunjia heshima kamati hiyo kwa kutoa taarifa fupi tu kuwa haitawakilishwa kwenye kikao chake cha usuluhishi.

Katika kikao hicho kamati hiyo pia  ilitoa uamuzi kwa malalamiko  ya kampuni ya Human Capital Investment Group Limited  dhidi ya gazeti la Rai   toleo namba 966 la April 5, 2012.Kuhusu malalamiko ya Lowassa kamati hiyo iliamua kuyasikiliza  upande mmoja baada kuarifiwa na  Kaimu Katibu wa Kamati kwamba  mwakilishi  wa Dira ya Mtanzania hatakuwepo kwa vile  mhariri wake Charles Mulinda  alikuwa safari.

Malalamiko ya Lowassa yaliyowasilishwa kupitia  mawakili wa kampuni ya  Imma advocates,  yalipokewa na  MCT Novemba 11, 2011.

Waziri mkuu huyo wa zamani alikuwa analalamikia zaidi ya habari sita ambazo zilimkashifu.
Habari ya kwanza  ilichapishwa katika  Dira ya Mtanzania toleo na 120 la Oktoba 6 – 9, 2011 iliyokuwa na kichwa cha habari  Lowassa, Chenge tena” ikifuatiwa na habari mbili  katika toleo na 123 la Oktoba 17-19, 2011   kwenye ukurasa wake wa kwanza  zikiwa na  vichwa vya habari  Nape atonesha kidonda – akumbusha Mwalimu  alivyomkataa Kapteni Lowassa na  Kapteni Lowassa atajwa kwenye  vurugu za CCM Arusha.

Katika toleo  la  125  la  Oktoba 24-26, 2011   ukurasa wa kwanza  gazeti hilo lilichapisha habari  Kapteni Lowasa, Kikwete basi.

Katika toleo la  Oktoba 31- Novemba 1, 2011  ukurasa wa kwanza  gazeti hilo lilichapisha habari yenye kichwa  Kapteni Lowassa  anaandaa mashitaka wakati katika toleo  128  la Novemba3-6, 2011 pia kwenye ukurasa wa kwanza, lilichapisha habari yenye kichwa  Askofu Mokiwa amkana  Kapteni Edward Lowassa.

Gazeti hilo pia lilichapisha habari kwamba CCM yapambana na Kapteni Lowassa 
Akiwasilisha shauri lake mbele ya Kamati hiyo ya  Maadili yenye wajumbe watatu, Lowassa alisema  kuwa maombi yake kadhaa ya kutaka kuweka sawa habari hizo na kuzikanusha  hayakushughulikiwa.

Alipoulizwa na Jaji  Mihayo  kwa nini  gazeti hilo lilifanya hivyo  licha ya juhudi zake, Waziri mkuu huyo wa zamani alisema  anafikiri lilikuwa linatumiwa ingawa sina ushahidi.
Hapo alisema anaomba  apendekeze kuwepo kwa sheria zitakazodhibiti  vyombo vya habari ambavyo vinakashifu watu makusudi kuwaharibia.

Kuhusu madai kuwa anakosana ana Rais Kikwete, Lowassa alisema  hiyo ni uhaini kutofautiana hadharani na  mkuu wa nchi.

“Kama rais angekuwa mtu mwingine anayefuata habari za magazeti unatiwa ndani”, alisema.
Jaji  Mihayo  alikubaliana naye kuhusu suala hilo la kumsema rais aliye madarakani  kuwa ni uhaini.Dira ya Mtanzania
 iliamriwa kumuomba radhi Lowasa na kumlipa fidia zote alizoingia katika shauri hilo.

Katika shauri lingine  gazeti la Rai limelalamikiwa kwa  kuchapisha katika toleo lake la  Aprili 25, 2012  kuwa TGNP yatapeliwa  270 mil/- Bagamoyo.  Yanunua kiwanja  kilichopo eneo la EPZ. Iliuziwa na kampuni  ya  Human Capital Investiment.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Zuhura  Muro  ambaye  aliiwasilisha   mbele ya kamati hiyo  alisema kuwa  taarifa ya gazeti hilo imeichafua kampuni hiyo na  vile  vile kumharibia sifa  yeye na hata familia yake. Mhariri Mtendaji wa New Habari inayochapisha gazeti hilo la Rai Prince Bagenda alikiri  kuwa  gazeti hilo lilikosea  na akaahidi kuchapisha taarifa ya kuomba radhi.Kamati hiyo ya MCT iliamuru kampuni hiyo kuomba radhi kwenye ukurasa wake wa kwanza..