Sunday, September 23, 2012

DAR GYMKHANA WAMTAKA MALINZI AGOMBEE UENYEKITI WA KLABU



Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi
----
Na Elizabeth John

WAKATI wanachama wa klabu ya Dar es Salaam Gymkhana, wakimtaka Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi kugombea nafasi ya Uenyekiti wa klabu hiyo, mwenyekiti aliyedaiwa kutimuliwa Ali Mafuruki, ameibuka na kudai kutoyatambua mapinduzi aliyofanyiwa.

Agosti 23 mwaka huu wanachama wa klabu hiyo walitangaza kumtimua, Mafuruki pamoja na wenzake na kuunda Kamati ya Muda inayomaliza muda wake madarakani hapo Septemba 28, watakapofanya uchaguzi, ambapo walimteua Victor Kimesera kuwa Mwenyekiti wa muda akisaidiwa na Erard Mutalemwa.

Mafuruki aliibuka na kudai kuwa ameshangazwa na kauli hizo za wanachama na kwamba yeye bado ni kiongozi wa klabu hiyo kwa mujibu wa katiba na uchaguzi wa viongozi uliofanyika Aprili mwaka huu, hali iliyozua mtafaruku baada ya Kimesera naye kudai kuwa yeye ndiye Mwenyekiti wa muda wa klabu hiyo.

Mafuruki alisema klabu hiyo inaendeshwa kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo ya mwaka 1952, na kusisitiza kuwa hakuna mtu aliyejiuzulu wala kutimuliwa wakati Kimesera alijibu kwa kudai kuwa klabu hiyo ni ya wanachama hivyo yeye amechaguliwa na wanachama kuwa mwenyekiti wa muda na ataendelea kushikiriawadhifa huo hadi hapo uchaguzi utakapofanyika Septemba 28 mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam jana Katibu wa muda wa Dar es Salaam Gymkhana, Adamu Ngamilo alisema kuwa viongozi wengine waliopendekezwa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Nichoraus Siwingwa, Kimesera na Abdalah Sykes.

Alisema waliopendekezwa kwa upande wa Makamu Mwenyekiti ni Elard Mtalemwa na yeye Ngamilo, pamoja na Jackson Mwaikinda.