Tuesday, September 18, 2012

ASKARI POLISI SINGIDA KIZIMBANI KWA KUSABABISHA VIFO VYA ASKARI WENGINE WATATU.


 

Bango la mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida.(Picha  na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Askari polisi dereva Idd Mvungi (33) mkazi wa Morogoro mjini amepandishwa kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mjini Singida, akituhumiwa kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha vifo vya askari polisi watatu wa kike na kujeruhi wengine sita.
Askari huyo amesomewa mashitaka yake akiwa amelazwa wodi namba tatu ya hospitali ya mkoa ambako anaendelea na matibabu.
Awali mwanasheria wa serikali Mary Mudulungu, alidai mbele ya hakimu wa mahakama ya mkoa Ruth Massamu, kuwa mnamo Septemba 14 mwaka huu saa 5.30 asubuhi eneo la Manguanjuki manispaa ya Singida, mshitakiwa Idd aliendesha gari PT 1149 aina ya Landrover defender kwa uzembe na kusababisha vifo vya askari polisi watatu wa kike na kujeruhi wengine sita.
Amesema siku ya tukio, mshitakiwa aliendesha gari hilo kwa uzembe na kitendo kilichochangia ashindwe kulimudu na gari lilienda kulia mwa barabara na kisha kupinduka.
Akifafanua, Mdulungu amewataja askari wa kike waliofariki kwenye ajali hiyo kuwa Rosemary Nyabukozi, Nywamwenda Juma na Neema Juma.
Aidha, mwanasheria huyo wa serikali, amewataja waliojeruhiwa kuwa ni MT 54597 SGT Juma, F.3523 PC Abdi, E.4943 D/CPL Kawawa, G.2842 PC Warioba, Johnbosco Sospeter na Bhoke Juma.
Mdulungu amemsomea shitaka la kumi kuwa mnamo septemba 14 mwaka huu saa 5.30 asubuhi huko eneo la Manguanjuki manispaa ya Singida, kuwa uzembe huo ulisababisha gari PT 1149 kuharibika.
Mshitakiwa anakabiliwa na mashitaka matatu ya kusababisha vifo, sita ya kusababisha majeruhi na moja la kusababisha uharibifu wa gari.
Mshitakiwa amekana mashitaka yote hayo na kesi yake itatajwa tena oktoba mosi mwaka huu.