CHAMA
cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema hakipo tayari kulipa gharama ya
hasara za uharibifu wa mali zilizotokana na mgomo wa walimu, kwa vile
hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa wao ndio waliohusika na uhalifu
huo.
Tamko
hilo linakuja ikiwa ni siku chache tangu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi, Dk. Shukuru Kawambwa, kulieleza Bunge kuwa CWT kama
waratibu wa mgomo huo, wanapaswa kulipa fidia za uharibifu wa jengo na
ofisi ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mji wa Tunduma na mali nyingine.
Akizungumza
na waandishi wa habari juzi mjini Tunduma baada ya kujionea uharibifu
wa ofisi hiyo iliyovamiwa na wanafunzi Julai 30 wakidai haki ya
kufundishwa, Kaimu Katibu wa CWT, Ezekiah Oluoch, alisema kama kuna
walimu walihusika moja kwa moja, serikali iwachukulie hatua.
“Ninachoweza
kusema kwa niaba ya CWT ni kutoa pole kwa uongozi wa mamlaka kwa
kuvunjiwa ofisi na kuibiwa samani na kikundi cha wahuni, na tunalaani
tukio lililotokea, lakini kwa sababu ofisi za CWT na mamlaka ni majirani
wema, tutakapopata tathmini ya uharibifu huo tutatoa kifuta machozi ila
si fidia ya ujumla, vinginevyo serikali itupeleke mahakamani,” alisema
Oluoch.
Aliongeza
kuwa, serikali haikitendei haki chama chao kwa kuwahusisha viongozi
wake kuwa wanafadhiliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kwa ajili ya kuvuruga amani ya nchi, na kwamba ikithibitisha suala hilo,
yeye atakuwa wa kwanza kujiuzulu wadhifa wake na kurudi kufundisha.
Kuhusu
sensa ya watu na makazi itakayofanyika hivi karibuni na kuwashirikisha
walimu, Oluoch alisema kuwa hawapo tayari kuwatetea walimu walioenguliwa
majina yao katika mchakato huo wa kusimamia sensa, na hivyo akawaonya
kujiepusha na vurugu zinazoweza kukwamisha.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mji wa Tunduma, Aidan Mwasiga,
alisema kuwa uharibifu uliotokea siku ya mgomo wa walimu, CWT hawawezi
kukwepa lawama kuwa chanzo, na kwamba suala hilo halihusiani na siasa.
Alizitaja
baadhi ya athari zilizopatikana bada ya ofisi yake kuvunjwa kuwa ni
pamoja na mji huo kukosa ushuru kutokana na nyaraka zote za kiserikali
kuibwa, vikiwemo vitabu vya kukusanyia mapato.
Source :Tanzania Daima