Sunday, August 12, 2012

Profesa Mahalu aachiwa huru



NewsImages/6564842.jpg
Prof. Mahalu akiwasiliana na ndugu na jamaa mara baada ya kuachiwa huru

ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, na aliyekuwa Ofisa wa Ubalozi huo, Grace Martine, wameachiwa huru baada ya kushinda kesi waliuokuwa wakikabiliwa na ufisadi dhidi yao
Jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwaachia huru baada ya ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka sita dhidi yao

Hukumu hiyo ilisomwa na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Illivin Mgeta, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa kwa pande zote mbili

Hakimu aliweza kutupilia mbali madai ya kutumia nyaraka mbalimbali kuidanganya serikali ili washitakiwa kujipatia fedha na kusema nyaraka zote zilizotumika zilikuwa halali kwa ajili ya ununuzi wa jengo la ubalozi huo lililogharimu Euro 3,098,741.40

Washitakiwa hao walikuwa wanadaiwa kuwa mwaka 2002 walikula njama ya kuiba Euro 2,085,827.60 kwa madai walinunua jengo la ubalozi mjini Rome, Italia kwa Euro 3,098,741.40 wakati lilinunuliwa kwa Euro 1,032.913.80.

Shahidi wa kwanza wa Jamhuri, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Martin Lumbanga, alitoa ushahidi wake kwa kudai hakuwa na taarifa ya ununuzi wa jengo la ubalozi nchini Italia na alipata taarifa hizo baada ya kusoma katika magezeti mbalimbali, na hakuwahi kutoa maelekezo ya kuandaa mikataba miwili tofauti ya kununulia jengo hilo.

Shahidi wa pili, Raia kutoka Rome, Italia, Marco Papi, aliyekuja nchini kutoa ushahidi, alikiri mahakamani kuwa alisaini mkataba mmoja ulioonyesha Euro milioni 1,032,000 baada ya kuhakikisha kuwa kuna makubaliano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa enzi hizo (JK), na Balozi huyo

Shahidi wa tatu, aliyekuwa Mhasibu wa ubalozi huo, Stewart Migwano, alidai kuwa aliandaa malipo ya ununuzi wa jengo kabla hajauona mkataba.

Mei 7, mwaka huu, Rais Mstaafu Mkapa, alikwenda fkutoa ushahidi wake na alidai alibariki ununuzi wa jengo hilo kwa mikataba miwili kama mmiliki alivyotaka.

Awali Profesa Mahalu na Grace walidaiwa kuwa Septemba 23, 2002 katika ubalozi wa Tanzania Rome, Italia, walimdanganya mwajiri wao kwa kughushi hundi ya malipo namba D2/9 yenye maelezo ya kununua jengo kwa Euro 3,098,741.58.

Ilidaiwa Oktoba Mosi, mwaka huo walitumia mkataba wa mauzo ukiwa na maelezo ya kughushi na walitumia hati hizo kuonyesha kuwa mmiliki wa jengo alipokea Euro 3,098,741.58.

Washitakiwa walifanya hivyo kwa lengo la kuipotosha serikali ya Tanzania na waliweza kuisababishia serikali hasara ya Euro 2,065,827.60 kwa kutumia vyeo vyao walivyokwua navyo kwa kipindi hicho.