Tuesday, August 21, 2012

MBEYA WASUBIRI LIGI KUU KWA HAMU KUBWA



 
Uwanja wa kumbukumbu ya sokoine jijini Mbeya


MENEJA wa uwanja wa Sokoine uliopo jijini Mbeya Modestus Mwaluka amesema maandalizi ya uwanja kwaajili ya ligi kuu ya Tanzania bara yamekamilika.

Amesema yapo maboresho makubwa yaliyofanyika katika uwanja huo na sasa upo katika kiwango cha ubora unaofaa kwa michuano mikubwa kama ligi kuu inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwanzoni mwa mwezi ujao.

Amesema miongoni mwa maeneo yaliyofanyiwa ukarabati ni pamoja na eneo la kuchezea(Pich) ambalo limejazwa udongo na kuoteshwa nyasi katika maeneo yaliyokuwa na mabonde hali ambayo awali ilikuwa ikisababisha usumbufu kwa wachezaji wakiwa katika mechi husika.

Meneja huyo amesema kwa maboresho yaliyofanyika kwa sasa uwanja uko katika hali nzuri na hata wachezaji wataona raha kuutumia tofauti na awali.

Kwa upande wa masuala ya usalama,Mwaluka amesema kwa sasa usalama wa wachezaji wawapo uwanjani,wale wa akiba pamoja na waamuzi na wahusika wengine ni mkubwa kutokana na wigo uliopo ambao katika siku za mechi ulinzi utaimarishwa zaidi ili mashabiki wasipate fursa ya kuingia eneo lisilowahusu.

“Mpaka sasa hatujapata ratiba lakini kwa taarifa tuilizonazo wakati wowote kuanzia leo itatoka.Kwa upande wetu kama wamiliki na wasimamiaji wa uwanja tumekamilisha mambo yote muhimu ikiwemo uboreshaji wa maeneo korofi.Tunachosubiri ni kuanza tu kwa ligi” amesema Mwaluka.

Hata hivyo baadhi ya wadau wa michezo jijini Mbeya wakiwemo wanahabari wameshauri uongozi wa uwanja kwa kushirikiana na chama cha soka mkoani Mbeya (MREFA) kuhakikisha unakuwepo utaratibu maalumu ambao hautaruhusu mamluki kuvamia eneo la wanahabari.

Katika ligi kuu ya Tanzania bara msimu huu,mkoa wa Mbeya na mingine iliyopo jirani itawakilishwa na timu ya Tanzania Prisons ya jijini hapa iliyopata daraja baada ya kufanya vyema katika michuano ya ligi daraja la kwanza iliyopita.

Kwa hisani ya Joachim Nyambo