Tuesday, August 07, 2012

MAONESHO YA NANE NANE KANDA YA NYANDA Z A JUU KUSINI, WAANDISHI WA HABARI WASUSIA KUANDIKA HABARI ZA MKOA WA MBEYA


 MKUU WA MKOA WA MBEYA ABBAS KANDORO

WAKATI maonesho ya siku kuu ya wakulima Nanenane mwaka huu 2012 kanda ya Nyanda za juu kusini yakiwa yamefikia siku ya sita katika viwanja vya maonesho hayo vya John Mwakangale Jijini Mbeya, waandishi wa habari wa mkoa wa Mbeya hawajaweza kuandika habari hata moja kuhusu maonesho hayo hasa wilaya za mkoa wa Mbeya.

Hali hiyo imegundulika baada ya waandishi wa mkoa huo kuelezea wazi hali iliyowafanya kutoweza kuandika habari za maonesho hayo hususani mabanda ya wilaya za mkoa wa Mbeya kwa kile walichosema kuwa kukosa ushirikiano wa dhati kutoka kwa wahusika na badala yake wamekuwa wakipata ushirikiano wa mikoa mingine hasa mkoa wa Katavi.

Waandishi waliohojiwa na kikosi kazi cha mtandao wa kalulunga.blogspot.com wamesema kuwa mbali na kutopata ushirikiano huo, pia posho zimekuwa zikigawiwa kwa upendeleo kwa baadhi ya waandishi wa habari ambao hata hivyo licha ya kupokea posho hizo hawajaweza kuandika habari za maonesho hayo kwa ujumla wake.

Uchunguzi wa uhakika usioacha shaka yeyote, umebaini kuwa Hali hiyo imepelekea ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya kujihoji yenyewe na kuomba kujua tatizo la kutoona habari yeyote kwenye mitandao, Redio, TV hata ya Serikali na Magazeti inayohusu Maonesho ya Nane Nane kutoka kwa baadhi ya waandishi wa habari ambao ina mahusiano nao.

Waandishi waliopigiwa simu na wengine kuitwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mbeya juu ya sintofahamu ya suala hilo, wamethibitisha kuwepo kwa hali hiyo na kwamba wameijibu kwa ufupi kuwa TASO imewakatisha tamaa kwa kutoa Sh.100,000 kwa baadhi ya waandishi na pia ofisi hiyo imechangia kwa kutoweza hata kuwapa hotuba ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro siku ya ufunguzi wa maonesho hayo.

Uhalisia wa baadhi ya waandishi wa habari kutokuwa na mahusiano mema na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya unajipambanua kwa msaidizi wa Mkuu wa mkoa ajulikanaye kwa jina la Masaya kuingilia majukumu ya afisa habari wa ofisi hiyo Sarah Mwakyusa ambaye anaoneka kumezwa na msaidizi huyo wa mkuu wa mkoa ambaye aliwahi kukalishwa kiti moto mbele ya aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo aliyepita John Mwakipesile kwa ubaguzi wa vyombo vya habari na waandishi wenyewe.

Hata hivyo baadhi ya waandishi wa Habari wengi wa mkoa wa Mbeya wamekubaliana kutoandika habari yeyote ya Maonesho ya Nanenane yanayohusu wilaya za mkoa huo bali kuendelea kuandika habari za wilaya za mikoa ya Rukwa, Katavi, Iringa na Ruvuma licha ya Ujumbe mfupi wa maandishi (SMS) kutoka kwa ofisa habari wa mkoa wa Mbeya kuomba wanahabari kuandika habari za mkoa huo mpaka mwisho wa maonesho hayo.