Tuesday, August 14, 2012

Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhardt Amtembelea Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad

  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiitikia dua baada ya kushiriki futari iliyoandaliwa na Masjid Iman iliyoko Mbweni Zanzibar.Katikati ni Sheikh Habib Ali Kombo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akifurahi pamoja na Balozi wa Marekani nchini Tanzania Alfonso Lenhardt, aliyefika nyumbani kwake Mbweni kwa ajili ya kubadilishana mawazo. Picha na Salmin Said-Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar 
---
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhardt ameahidi nchi yake itaunga mkono juhudi za Zanzibar kuwa na mipango madhubuti ya uokoaji wakati yanapotokea majanga, ili kunusuru maisha ya watu pale inapotokea hali kama hiyo.

 Amesema msaada wa Marekani utaelekezwa zaidi kuiwezesha Zanzibar kuwa na mfumo wa kisasa wa mawasiliano utakaosaidia kujua eneo la tukio na kumudu kufika kwa haraka, kwa nia ya kuokoa maisha ya watu wengi zaidi iwezekanavyo. 

 Balozi Alfonso amesema hayo leo alipokuwa na mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad huko nyumbani kwake Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar kuzungumzia tukio la kuzama kwa meli ya MV. Skagit, pamoja na mambo mengine mbali mbali. “Msaada huu wa kuepusha maafa wakati yanapotokea majanga, utakuwa ni kwa Tanzania nzima, lakini tutahakikisha Zanzibar inanufaika nao na inajijengea uwezo wa kuokoa maisha ya watu wake, wakati wa maafa kama haya ya kuzama kwa meli na mengineyo”, aliahidi Balozi Lenhardt. 

 Hata hivyo, Balozi huyo wa Marekani alisifu mshikamano wa wananchi wa Zanzibar pamoja na serikali yao, wakati wa maafa ya kuzama kwa MV. Skagit mwezi uliopita, hali ambayo ilisaidia kuokolewa baadhi ya watu waliokuwemo kwenye meli hiyo. 

 Naye, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amekaribia azma hiyo ya Marekani kuisaidia Zanzibar katika kukabiliana na majanga mara tu yanapotokea. Katika hatua nyengine Balozi Lenhardt ameisifu Zanzibar kwa hatua kubwa iliyoweza kufikia kudhibiti ugonjwa wa Malaria ambao umekuwa ukisababisha vifo vya watu wengi wakiwemo watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

 Balozi huyo amesema Zanzibar imejijengea heshima na hivi sasa imekuwa mfano Duniani na wataalamu kutoka sehemu mbali mbali wanakuja Zanzibar kujifunza mbinu za kutokomeza ugonjwa huo. Akizungumiza mafanikio hayo, Maalim Seif alisema suala la elimu kwa wananchi juu ya kutokomeza ugonjwa huo limechangia kwa kiasi kikubwa kuwa na uelewa wa hali ya juu kujilinda wasipate maradhi hayo. 

 Maalim Seif alisema baada ya wananchi walio wengi kuelewa mbinu za kujikinga na Malaria imekuwa rahisi kuweza kuzitumia njia wanazoshauriwa na wataalamu. 

 Alizitaja baadhi ya mbinu hizo kuwa ni matumizi ya vyandarua, kupuliziwa dawa kwenye nyumba zao, kuweka mazingira yao katika hali ya usafi pamoja na kufika kwenye vituo vya afya kwa uchunguzi na kutibiwa mara wanapoona dalili za kuwa na maradhi hayo. 

 Balozi huyo wa Marekani pia amemhakikishia Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa nchi hiyo itaendelea kufanikisha miradi mbali mbali inayofadhiliwa na Marekani hapa Zanzibar. 

 Miongoni mwa miradi hiyo ni utandikaji wa laini kuu ya umeme kutoka Dar es Salaam hadi Fumba kupitia chini ya bahari na ujenzi wa barabara tafauti, ambayo yote ipo katika hatua nzuri za utekelezaji. 

 Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais jana alijumuika katika futari iliyoandaliwa na masjid Iman iliyoko mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar. 

 Futari hiyo iliwajumuisha wananchi mbali mbali wanaosali katika msikiti huo pamoja na viongozi kadhaa wa dini na siasa wakiwemo Sheikh Habib Ali Kombo na Makamu Mwenyekiti wa CUF Machano Khamis Ali.
 
Na
 Hassan Hamad
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar