Friday, August 17, 2012

ACT YAMPA TUZO JK.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal akionyesha tuzo ya Mh. Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliyopokea kwa niaba yake.

Na Mwandishi Wetu

Baraza la Kilimo la Tanzania (ACT), limempa Tuzo Rais Jakaya Kikwete, kutokana kuutambua mchango wako katika kukuza maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.

Mwenyekiti wa ACT, Salum Shamte, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema Madhumuni ya kutoa Tuzo hii tunayoiita 'Tuzo ya Kilimo kwanza' ni kuuenzi mchango na jitihada zake binafsi na za Serikali kwa ujumla katika kuinua sekta ya kilimo na wakulima nchini.

"Aidha, kupitia Tuzo hiyo, tutakuwa tunawatambua waliochangia kuleta Mapinduzi ya Kilimo kwa manufaa ya Wakulima wa Tanzania"alisema

Alisema ni matarajio ya ACT kuwa Tuzo hiyo itahamasisha viongozi na wadau wengine kuiga mfano wako na, kuongeza nguvu katika kufanikisha malengo ya Taifa ya kukuza kilimo, ufugaji na uvuvi na kuondoa umasikini.

Mwenyekiti alisema Tuzo pia itahamasisha wazalishaji na wadau wengine wa sekta ya kilimo kutumia fursa kubwa iliyopo wakati huu ya kuongeza uwekezaji wao kwa mbinu mbalimbali za kisayansi na kiteknologia kwa ajili ya kuongeza tija na kipato cha wananchi na kujenga uchumi imara wa Taifa letu.  

Aliongeza kwamba, Rais Kikwete anastahili Tuzo hiyo kutokana na mchango wake katika Sekta hiyo tangu alipoingiza madarakani.

Alitaja michango aliyoifanya Rais ni pamoja na kukipa kipaumbele kilimo katika ya Agenda ya uchumi kitaifa kwa kuzindua Azma ya Kilimo Kwanza, ambapo Azma hiyo ilitokana na mchakato adhimu wa miaka mitatu  wa mashauriano baina ya Serikali na Sekta Binafsi ikiwaunganisha wakulima, wafugaji na wavuvi.

Aidha, aliongeza kuwa Rais pia ameongeza bajeti ya kilimo kutoka wastani wa asilimia 2.2 ya bajeti ya Serikali  kabla hujaingia madarakani, hadi kufikia asilimia 9 mwaka huu wa fedha.

Hata hiyo Rais amefanikiwa kutekeleza kwa umakini mkubwa Programu Kabambe ya Maendeleo ya Kilimo (ASDP) nchini , Programu hiyo ya miaka saba iliyoanza kutekelezwa mwaka 2006, ina madhumuni ya kuongeza tija ya wakulima na kuweka mazingira bora kwa sekta binafsi ya kuwekeza katika kilimo.

Shamte alisema kuna kila sababu ya kumpa Tuzo Rais kwa kuweka kuingiza matrekta kwa wingi ili kupanua eneo la kilimo na hatimaye kuondokana kabisa na kilimo cha jembe la mkono ambapo imeziwezesha taasisi za Serikali za SUMA JKT na Mfuko wa Taifa wa Pembejeo kusambaza zana za kilimo kwa wakulima kwa mikopo yenye masharti nafuu.

Hivyo, alisema mfano unaostahili kuigwa na viongozi na wananchi wengine, kwani wahenga walisema, 'ada ya mja kunena, muungwana ni vitendo'.