Picha ya Bashar al Assad ikiraruliwa
Aliyekua Mkuu wa ujumbe wa
waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Jenerali Robert Mood
amesema utawala wa Rais Bashar Al Assad unakaribia kufika ukingoni.
Jenerali Mood mwenye uraia wa Norway amesema
machafuko ya sasa yanazidi uwezo wa majeshi ya serikali huku mauaji ya
raia yakiendelea kwa kiwango kikubwa, hali inayodidimiza matumaini ya
majaaliwa ya Utawala wa Bw. Assad.Hata hivyo ameonya kwamba machafuko yataendelea hata kama utawala wa sasa utaanguka.
Wafanyakazi wa shirika la msalaba mwekundu wakiwasaidia wakimbizi
Huku haya yakiarifiwa Shirika la Msalaba Mwekundu limewaondoa maafisa wake kutoka mji wa Aleppo huku likiomba masaada wa damu kuokoa maisha ya majeruhi.
Majeshi ya serikali yameendelea kuelekea eneo hilo kwa silaha nzito na inahofiwa kutokea makabiliano makali kati ya vikosi tiifu kwa serikali na waasi.
Maeneo mengi ya Aleppo yamelengwa usiku kucha kwa makombora ya kijeshi.
Wakati huo huo Kamishina wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu , Navi Pillay, ameelezea wasi wasi wake kuhusu usalama wa raia katika makabiliano yanayoendelea.
Mwandishi wa habari wa gazeti la Ufaransa Le FigaH'o Adrien Jaulmes yuko Aleppo na amekua na waasi. Akiongea na BBC mwandishi huyo amesema waasi wameelezea matumaini ya kuwazidi nguvu majeshi ya serikali.
Chanzo: BBC