Saturday, July 28, 2012

TAMKO LA WAFANYAKAZI WA MTANDAO WA VIKUNDI VYA WAKULIMA TANZANIA (MVIWATA) KUHUSU MABADILIKO YA SHERIA YA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII

TAMKO LA WAFANYAKAZI WA MTANDAO WA VIKUNDI VYA WAKULIMA TANZANIA (MVIWATA) KUHUSU MABADILIKO YA SHERIA YA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII
27 Julai 2012
 
Sisi wafanyakazi wa MVIWATA tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya mabadiliko ya  sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii yaliyofanywa na bunge mwezi Aprili mwaka 2012 na kusainiwa na Mheshimiwa Rais  Jakaya Kikwete yanayomtaka mfanyakazi kulipwa mafao yake baada ya kufikisha umri wa miaka 55 hadi 60.
 
Kwanza, tunashangazwa iwapo kweli dhamira ya mabadiliko hayo ni kuboresha maslahi ya mfanyakazi na tunatilia shaka hoja hiyo. Mchakato uliotumika kuibua sheria hiyo ambao ulikosa uwazi, taarifa zilizopo juu ya hali ya kifedha ya mifuko yenyewe pamoja na uendeshaji wa mifuko hata kabla ya mabadiliko hayo yanadhihirisha kwamba dhamira ya marekebisho ya hayo si kwa maslahi ya mfanyakazi.

Kwa hiyo, tukiwa wafanyakazi wa sekta binafsi, tunaungana na wafanyakazi wenzetu katika sekta hii wanaopinga kwa nguvu zote sheria  hii ambayo utekelezaji wake hautakuwa na manufaa kwetu wafanyakazi, kwa sababu zifuatazo;
 
1.     Ajira zetu ni za mikataba ya muda mfupi na zisizo na uhakika, hivyo mafao ya kujitoa yanamsaidia mfanyakazi kama mtaji (kianzio cha maisha) mara baada ya kumaliza mkataba wake au kuacha kazi.
2.     Tukiwa wafanyakazi wa ajira za mikataba ya muda mfupi mfupi hatuna uhakika wa kupata kazi nyingine mara baada ya kumaliza mikataba yetu na hivyo kutulazimisha kusubiri hadi kufikia miaka 55 ni kutunyima haki zetu za msingi za kuishi maisha bora. Haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyang’anywa!!
3.     Mchakato mzima wa kupitisha mswada mpaka kusainiwa kwa sheria hii haukutushirikisha wamiliki wa mifuko hiyo ambao ndiyo wachangiaji.
4.     Kwa sababu ya urefu wa muda hadi kufikisha miaka 55-60 na kwamba mifuko hii ya jamii haina riba, fedha atakayopatiwa mchangiaji atakapostaafu haiwezi kuwa na thamani iliyonayo wakati anachangia. Katika hali hiyo malipo ya uzeeni hayamsaidii mchangiaji kupunguza ugumu wa maisha kama ilivyoelezwa katika ufafanuzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii - Social Security Regulatory Authority (SSRA).
5.     Uzoefu wa wastaafu waliokuwa  wafanyakazi wa Jumuia ya Afrika Mashariki ambao wamepoteza haki zao mpaka leo unatufanya tusiiamini mifuko ya hifadhi ya jamii.
 
Kwa hiyo, sisi wafanyakazi wa MVIWATA tunatamka kwa kauli moja kwamba;
1.     Hatukubaliani na mabadiliko hayo ya sheria na tunapinga vikali utekelezwaji wa sheria ya fao la kujitoa kwani ni kandamizi.
2.     Tunaitaka serikali ifute mara moja sheria hii kandamizi yenye lengo la kutunyima wafanyakazi haki zetu na kutupora maisha yetu.
3.     Tunaunga mkono wabunge wanaotaka sheria hii ijadiliwe na kurekebishwa ili kulinda maslahi ya wafanyakazi.
4.     Tunakusudia kusitisha michango yetu katika mifuko ya hifadhi ya jamii iwapo sheria hii haitaondolewa.
 
Susuma Susuma,
Communication Officer
Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA)
E-MAIL: susuma9@yahoo.com, susuma9@hotmail.com, www.mviwata.org
Mobile +255 754 652 773
Tel. +255 23 2614184
Fax. +255 23 2614184
Morogoro