Kaimu Mkurugenzi
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar Abdullah Husein Kombo wakati alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari Afisini kwake leo Malindi Mjini
Zanzibar-Picha na Nafisa Madai-Maelezo Zanzibar
--
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
26/07/2012
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar imezifutia rasmi hati ya
kufanya kazi Meli ya Mv.Kalama, Mv.Seagul na Mv.Sepideh kutokana na meli hizo kutokukidhi
hali ya usalama wa abiria katika meli hizo. Aidha meli hizo zimepewa muda
wa mwezi mmoja kuanzia leo kuhakikisha zimeondoka katika maeneo ya Zanzibar
kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi ya wamiliki wa Meli hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Usafiri wa
Baharini Zanzibar Abdullah Husein Kombo wakati alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari Afisini kwake kuhusu hali ya usafiri wa baharini na usalama
Zanzibar. Amesema Mamlaka hiyo imefanya tathmini na uhakiki wa kutosha na
kujiridhisha kuwa Meli hizo hazifai kufanya kazi katika maeneo ya Zanzibar
jambo ambalo limepelekea kuchukua hatua za kufuta hati za kufanyia kazi meli
hizo.
Amefahamisha kuwa sababu kuu zilizopelekea Mamlaka kufanya maamuzi
hayo ni pamoja na uchakavu,umri wa meli hizo kuwa mrefu na kupata matatizo mara
kwa mara katika safari zao. Kombo amefahamisha kuwa Sheria ya Mamlaka ya
Usafiri na Bandari Zanzibar ya mwaka 2006 kifungu cha 17.1 inampa mamlaka
Msajili wa Meli kuifuta meli yoyote ambayo itakuwa haikidhi usalama wa abiria.
Kufuatia sheria hiyo Kombo amesema watawataka wamiliki wa Meli
hizo kuzirudisha hati za kufanyia kazi meli hizo ili waende kutafuta sehemu
nyengine za usajili kinyume na maeneo ya Zanzibar. Akizungumzia Meli ya
Mv.Serengeti Kombo amesema wamelazimika kuiagiza meli hiyo kupunguza idadi ya
abiria kutoka watu 800 hadi 350 na tani za mizigo kutoka 100 hadi 50 hadi
pale ambapo watajiridhisha kutokana na hali ya meli hiyo ilivyo.
Aidha amegusia kuwa Kampuni ya Bakhresa italeta Meli kubwa ya
abiria itakayofanya kazi zake Zanzibar ambapo pia Serikali ya Mapinduzi nayo
iko mbioni kuhakikisha wanaleta meli inayokidhi mahitaji ya wananchi wa
Zanzibar.