
Mkurugenzi wa Tanzania One Thetre (TOT) ambaye pia ni Mbunge wa
Mbinga Magharibi, John Komba akizungumzia hali ya afya yake, alipowaita
waandishi wa habari, nyumbani kwake, Mbezi Tangi Bovu, Kawe, Dar es
Salaam, leo, Julai 27, 2012. Kushoto ni Mkewe, Salome Andrew KombaPicha na Mpiga Picha Wetu
--
NA BASHIR NKOROMO
MKURUGENZI wa Kundi la Tanzania One
Theatre (TOT) ambaye pia ni Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba
amerejea kutoka India ambako amefanyiwa upasuaji kumtibu ugonjwa wa
nyonga ulilokuwa ukimsumbua upande wa mguu wake wa kulia.
Akizungumza na waandishi wa habari, jana Julai 27,
2012, nyumbani kwake Mbezi kwa Komba, mjini Dar es Salaam, Komba alisema
amerejea nchini, Juzi, baada ya kupatiwa matibabu hayo kwenye
hospitali ya Appolo iliyopo Hydrabad nchini India tangu mwanzoni mwa
wezi huu.
Alisema, aliondoka nchini, Julai 2, 2012, baada ya
kupelekwa na serikali kwa maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete, Spika wa
Bunge Anna Makinda na Katibu wa Bunge John Kashilila na kwamba alikwenda
baada ya kukosa matibabu hapa nchini kwa sababu ya mgomo wa madaktari.
"Siku napelekwa Muhimbili tu, tayari madaktari
walikuwa wameanza siku ya kwanza ya mgomo wao, nikawa sina namna ila
kuujulisha uongozi wa Bunge na kisha nikamuomba Mwenyekiti wa CCM, Rais
Jakaya Kikwete, naye kwa mamlaka yake akanisaidia haraka kama ambavyo
huwasaidia wengine kwenda kutibiwa nje", alisema Komba.
Alisema, uzito ulichangia sana kusababisha mifupa
kusagana kwenye nyonga upande wa mguu wa kulia, ambapo hadi anakwenda
India alikuwa na uzindo wa kilo 138 wakati wastani wa uzito aliotakuwa
kuwa nao kulingana na ukumbwa wa mwili wake ni kilo 90 au 100 tu.
"Amesema, baada ya matibabu amerejea nchini akiwa na
uzito wa kilo 128 ambao hata hivyo ametakiwa kuudhibiti na kuupunguza
katika siku hizi ambazo atalazimika kupumzika nyumbani kabla ya kuanza
kazi, Mwezi Septemba mwaka huu kama alivyoelekezwa na madaktari.
Akizungumzia upasuaji ulivyoendeshwa, Komba alisema,
ulichukua saa tano na kukamilika bila matatizo katika upasuaji huo
ambao alisema sehemu iliyopasuliwa ni ya ukumbwa wa futi moja.
Alisema, hata hivyo baada ya upasuaji huo, hakuweza kurejea katika
wodi ya kawaida, kwa sababu majongwa kadhaa yaliibuka ikiwemo homa kali,
presha, hivyo akalazimika kulazwa katika wodi ya wagonjwa waliopo
kwenye uangalizi maalum (ICU) kwa siku tano.
"Sasa nimerejea nikiwa mzima, kwa sasa natumia fimbo
hii, ili kuwezesha uzito uzilemee upande wa kulia nilikopanyiwa
upasuaji, lakini sijambo kabisa", alisema Komba.
Komba alilaani baadhi ya vyombo vya habari ambavyo viliripoti kwamba
katika kuugua kwake alikuwa mahututi na kwamba alikuwa anaugua figo.
"Jamani
ninyi waandishi wa habari, jizoesheni kuandika habari zilizokamilika
siyo kurashia-rashia tu na kuzusha uongo, mfano gazeti moja liliandika
eti naugua figo nipo mahututi, wakati si kweli kabisa, ilikuwa jambo
rahisi tu, kuja hapa nyumbani na kuniuliza au kuuliza mke wangu
lingepata kwa uhakika ninachoumwa", alisema Komba.
Mwisho.