Siwezi kukulaumu wewe na Mamlaka unayoisimamia, wakulaumiwa ni wa Wabunge. Labda hawakusoma vizuri, lakini wewe ni timu yako naamini ndo chanzo cha Sheria hii. Hisia zangu na wafanyakazi waliowengi, kama unavyoona makelele, sijarizika kabisa na hatua hii! Mimi ni mfanyakazi na hata huo ufafanuzi wako wa Julai 20, 2012 nimeusoma, haikidhi kiu ya kuamini kwamba FAO LA KUJITOA kufutwa kunafaida yoyote ukiondoa fursa ya kukopa nyumba!!!??? SSRA inasisitiza eti tuelimishwe, Hatuelimishiki katika hili! "Mla Mla Leo bwana Mla Kesho Kala nini?" Sisi wenye vipato vya chini tunafanya maendeleo kupitia vijisenti hivyo; tunasomesha, tunajenga kwa awamu, tunajisomesha wenyewe. Sasa mnatupeleka wapi?
Maisha ya Mtanzania ni ya kubahatisha; wachache wanapita hadi uzee, ndo maana tunawazee wachache. Wastani wa kuishi kwa Mtanzania wa leo ni Miaka 58 na miezi miwili tu. Sisi mnatutaka kufikishe 55 ili tuishi miaka 3 tu kisha tufe!! Natukitaka kuendelea na kazi hadi miaka 60 tutakuwa tumekufa hata kabla ya kuchukua mafao hayo.Bado kuna magonjwa mengi sana yanayoua mara moja ikiwemo VVU/UKIMWI, lo! Achilia mbali ajali za mala kwa mala; yote haya yanaashilia kwamba tutafanyia kazi kwaajili ya Miradhi ya watoto wetu tu, au waume zetu/wake zetu wakibahatisha kufika. MLA MLA LEO mkuu.
Fedha ya nchi yetu pendwa, Tanzania ni ya kuporomoka kila kunapokucha! Mamlaka yako pamoja na Bunge mnatutaka tutunze hayo makaratasi hadi uzeeni, huku thamani nayo inaporomoka! Ninahitaji maelezo zaidi hapo yakihusisha thamani ya pesa yetu na kuporomoka kwake na MAfaho ya Uzeeni.
Ndugu Mkurugenzi, "Kupanga ni Kuchagua", Mwalimu Nyerere alisema. Mbona sisi hatujachagua kujitoa? Mbona hatukushirikishwa kikamilifu. SSRA imekimbilia kurubuni wafanyakazi eti "ili kutimiza lengo na mathumuni ya hifadhi ya jamii ambayo ni kuhakikisha kuwa mwanachama anapata mafao bora". Mafao bora menyewe hayajawahi kutolewa. Tumeona ndugu zetu, watangulizi wetu akipokea vijihela kiduchu tu! Njia iliyotumika kushirikisha wafanyakazi hakukidhi haja na mahitaji halisi ya wafanyakazi. Wabunge hatukuwatuma hilo, jamani. Haya ndo matatizo ya uakilishi. Mwakilishi anajiamulia tu ya kusema Bungeni, bila kukusanya maoni halisi ya anaowawakilisha.
Hata SSRA ambayo naamini ndio chanzo cha maudhi haya yote haikufanya utafiti wa kutosha kuhusu mahitaji halisi ya wafanya kazi. Mahitaji siyo nyumba pekee. Na si kila mtu anataka kukopa nyumba. Wengine tunataka hela tuanzishe maduka, wengine tunataka twende kusoma tukiwa ngali vijana. Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii tunaitumia kujiwekea akiba wenyewe na pindi malengo yetu akikamilika tunazitoa na kuzifanyia kazi tulizopanga. Enzi hii, siyo Enzi ya Mwalimu! Ni enzi ya soko huria likiwemo Soko Huria la Ajira. Mtu anauwezo wa kujenga nyumba hata kama si mfanyakazi wala si mfanya biashara! Wafanyakazi si mbumbumbu kiasi cha kulazimishwa kujiwekea fedha. Hebu tuachwe tuamue mambo yetu wenyewe.
Binafsi sioni faida ya Mifuko hii nje ya FAO la Kujitoa. Siwezi hata kukopa fedha mfano NSSF wakati wao wanatumia fedha zangu ninazoendelea kuweka kujenga majumba ya kitega Uchumi pasipo mimi kupewa Mgao hata kidogo angalao. Faida yoooote inakwenda NSSF. Mimi faida yangu ni mafao madogomadogo tu, kama vile matibabu kiduchu, Kifo (wala sitafaidi). FAO la kujitoa ndo lenyewe kwa Mfanyakazi. Mla Mla Leo.
Mikataba yetu ni ya muda mfupi-Miezi Sita, Mwaka Mmoja, Miwili, nk. Katyika hali hii unanitaka ni subiri hadi Miaka 55 kwa mafao yangu ya miaka Miwili au Mitano!? Hii sheria labda tuwaachie watumishi wa Serikali ambao wan mikataba ya muda mrefu, hadi umri wa miaka 60. Sekta zingine haiwezekani.
Nawasilisha,
Mhangwa, Vincent Manoni
+255 782 396953