Friday, June 22, 2012

Miujiza - Mwanaume Aliyekatwa Miguu Apanda Mlima Kilimanjaro Kwa Mikono



NewsImages/6479046.jpg
Spencer West akishangilia kufika kilele cha mlima Kilimanjaro kwa kutumia mikono yake
Thursday, June 21, 2012 3:12 PM
Huenda ikaonekana ni kama miujiza lakini kitu ambacho kimewezekana, mwanaume ambaye alikatwa miguu yake yote miwili alipokuwa mdogo, ameushangaza ulimwengu kwa kupanda mlima Kilimanjaro hadi kileleni kwa kutumia mikono.
Mwanaume raia wa Kanada, Spencer West mwenye umri wa miaka 31, amekuwa gumzo duniani kwa kuweza kuupanda mlima Kilimanjaro kwa kutumia mikono yake hadi alipofika kileleni.

Spencer alikatwa miguu yake yote miwili alipokuwa na umri wa miaka mitano kutokana na magonjwa yaliyomkumba baada ya kuzaliwa.

Spencer alifanya mazoezi ya kupanda mlima Kilimanjaro kwa muda wa mwaka mmoja na aliwasili Tanzania juni 21 mwaka huu akiwa na marafiki zake wawili.

"Wakati tunakikaribia kilele baada ya siku saba za kupanda futi 20,000 za mlima Kilimanjaro tukitokwa jasho, damu, tukitapika wakati mwingine hatimaye tumefanikiwa kufika kileleni", alisema Spencer.

Spencer aliupanda mlima kilimanjaro kwa kujiburuza kwa mikono yake huku asilimia 20 tu ya safari yake hiyo akitumia baiskeli yake ya vilema.

"Damu iliyomwagika toka kwenye vidole vyangu na majipu yaliyojitokeza vidoleni yote si kitu kama kufanikiwa kufika kilele cha mlima Kilimanjaro", aliongeza Spencer.

Ni asilimia 50 tu ya watu wanaojaribu kuupanda mlima Kilimanjaro hufanikiwa kufika kileleni. Bilionea wa Chelsea, Roman Abramovich ni miongoni mwa maelfu ya watu waliojaribu kuupanda mlima Kilimanjaro wakaishia njiani bila ya kufika kileleni.

"Nimeamua kuupanda mlima Kilimanjaro si kuwaonyesha watu nini naweza kufanya bali ni kuwapa changamoto watu kuwa pamoja na matatizo yanayowakabili wanaweza kufanya vile vinavyoonekana haviwezekani", alisema Spencer.

Safari ya Spencer kupanda mlima Kilimanjaro imesaidia kuingiza paundi 300,000 ( Zaidi ya Tsh Milioni 750) ambazo zitatumika kusaidia watoto wanaohitaji misaada nchini Kenya.