Thursday, April 12, 2012

Dk. Mwakyembe alitikisa Bunge

Dk. Mwakyembe alitikisa Bunge


Mbunge wa Kyela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Mbunge wa Kyela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, jana alipokelewa kwa mbwembwe na wabunge wenzake aliposimama kwa mara ya kwanza kujibu maswali ya wizara yake.

Dk. Mwakyembe alishangiliwa kwa nguvu na wabunge hao wakati wa kipindi cha maswali na majibu aliposimama kujibu swali la Mbunge wa Rorya Lameck Airo (CCM), aliyetaka kujua utekelezaji wa ahadi ya Rais kuhusu ujenzi wa barabara ya Mika-Utegi-Randa na Shirati.
Dk. Mwakyembe alipelekwa nchini India kwa matibabu mwishishoni mwa mwaka jana kwa ajili ya matibabu ya maradhi ya saratani ya ngozi.
Kabla ya kujibu swali hilo, Naibu Spika, Job Ndugai, alimkaribisha Dk. Mwakyembe kujibu swali bungeni ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu aende kutibiwa nchini India zaidi ya miezi mitano iliyopita.
Kabla ya kuanza kujibu maswali ya wizara yake, Dk. Mwakyembe alitumia muda mwingi kuwashukuru Watanzania waliomwombea wakati wote wa kuugua kwake hadi kupata nafuu na kurejea nchini.
Aliwashukuru Spika wa Bunge, Anne Makinda; Naibu Spika, Job Ndugai na wabunge wote wa vyama vyote kwa kumjulia hali na kufuatilia hali yake.
Alimshukuru Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya afya yake tangu alipokwenda kutibiwa nchini India hadi aliporejea.
“Nawashukuru watanzania wote Wakiristo na Waislamu kwa kuniombea muda wote bila kuchoka, Mungu amewasikia na leo mnaniona ni mzima wa afya na niko salama, nawashukuru pia wapiga kura yangu wa Kyela ambao hivi karibuni walinipa mapokezi makubwa,” alisema Dk. Mwakyembe.
Akijibu swali kuhusu ahadi zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 za ujenzi wa barabara mbalimbali nchini, Dk. Mwakyembe alisema ahadi zote za Rais ni lazima zitekelezwe, lakini utekelezaji huo unafanyika kwa awamu.
“Ahadi zote za Rais zitatekelezwa, lakini ikumbukwe kuwa ahadi hizo ni hadi mwaka  2015, ziko nyingi hivyo haziwezi kutekelezwa kwa mwaka mmoja tu,” alisema.
Kuhusu ujenzi wa barabara ya Serengeti, Dk. Mwakyembe alisema serikali imeahidi kuijenga kwa kiwango cha lami na itafanya hivyo wakati ukifika.


Joseph Mwendapole na Sharon Sauwa, Dodoma
CHANZO: NIPASHE