Mbunge wa Jimbo la Ubungo (CHADEMA), Mhe. John Mnyika.
Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kufukuzwa kwa wanafunzi 13 wa  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wakiwemo viongozi wa Serikali ya  Wanafunzi (DARUSO) na wengine 86 kusimamishwa masomo kuanzia tarehe 10  Januari 2011.
 Kutokana na hali hiyo nakusudia kukutana na uongozi wa  Chuo Kikuu cha Dar es salaam kufanya mazungumzo ili maamuzi hayo yaweze  kubadilishwa na iwapo hatua muafaka. Iwapo ufumbuzi wa mapema  hautapatikana pamoja na kuchukua hatua zingine za kibunge  nitakazozieleza baadaye nitatoa mwito kwa Rais Jakaya Kikwete kuingilia  kati kwa kuwa matatizo katika vyuo vikuu kwa sasa yamechangiwa na  udhaifu wa kiutendaji katika Serikali.
 Ikumbukwe kwamba Waziri wa  Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dr Shukuru Kawambwa aliahidi bungeni kwenye  mkutano wa nne kwamba serikali imepata mkakati wa kumaliza migogoro na  matatizo katika vyuo vikuu nchini na kwamba hatua za haraka  zingechukuliwa kama sehemu ya utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa  mwaka 2011/12.
 Hata hivyo, badala ya migomo na migogoro kumalizika  inaelekea kuongezeka na kufikia kiwango cha wanafunzi kufukuzwa na  wengine kusimamishwa katika vyuo vikuu mbalimbali vya umma ikiwemo Chuo  Kikuu Cha Dar es salaam (UDSM),  Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi  Shirikishi (MUHAS) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
 
 Kwa mujibu  wa ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  mamlaka ya bunge ni kutunga sheria na kusimamia serikali. Kutokana na  mamlaka hayo kazi za mbunge ni kuwakilisha wananchi, kushiriki katika  kutunga sheria pamoja na kuisimamia serikali na viongozi wake. Hali  katika vyuo vikuu hivi na vingine haiendani na ahadi ambayo Waziri  Kawambwa alizitoa bungeni na kwa umma miezi kadhaa iliyopita.
 
  Kutokana na hali hiyo tarehe 12 Desemba 2011  niliwasiliana na wizara  yenye dhamana ili iweze kuingilia kati kama sehemu ya kutimiza ahadi  iliyotolewa bungeni hata hivyo hatua muafaka hazikuchuliwa.
 Katika  kukabiliana  migomo na migogoro katika elimu ya juu serikali imekuwa  ikichukua hatua dhidi ya matokeo badala ya kushughulikia vyanzo vya  matatizo hivyo natarajia wakati huu Waziri husika atajielekeza katika  madai ya msingi ya wanafunzi na wahadhiri.
 
 Serikali itambue  kwamba chanzo cha migomo ya hivi karibuni UDSM ni kugeuzwa kwa taratibu  za utoaji mikopo na hatimaye kuchelewa kwa malipo ya wanafunzi na  wengine kupata pungufu au kukosa kabisa. Katika mazingira hayo  nasisitiza kwamba ni muhimu kwa Waziri Kawambwa kuweka wazi kwa umma  ripoti ya Tume ya Rais iliyoundwa tarehe 14 Februari 2011 na kukabidhi  taarifa yake tarehe 29 Aprili yenye mapendekezo ya jinsi ya kuboresha  utaratibu wa sasa wa ugharamiaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya  elimu ya juu.
 
 Kuwekwa wazi kwa taarifa hii kutawezesha  wawakilishi wa wananchi, wanafunzi, wazazi, vyuo vikuu na wadau wengine  wote kuunganisha nguvu katika kushughulikia matatizo yanayoendelea  kujitokeza katika elimu ya juu hivi sasa.
 Ikumbukwe kwamba Rais  Jakaya Kikwete aliahidi mwaka 2007 kuyapatia ufumbuzi matatizo ya  wanafunzi wa elimu juu nchini ili kupunguza migomo na migogoro. Katika  Mkutano wake na wanafunzi wa vyuo vikuu mwezi Februari 2007 alikwenda  mbali zaidi kwa kuwaeleza kwamba hakuna mtoto wa maskini atayeshindwa  kuendelea na masomo kutokana na masharti ya mikopo.
 
 Miaka  mitano imepita toka ahadi hizo zitolewe migomo katika vyuo vikuu  inaendelea na pia wapo watoto wa walalahoi ambao wamefaulu kidato cha  sita lakini wemeshindwa kuendelea na masomo kutokana na kukosa mikopo;  hivyo Waziri asipochukua hatua za haraka itadhihirika kwamba ahadi za  serikali zimekuwa za 'kiini macho'.
 
 Izingatiwe kuwa kwa mujibu  wa ibara ya 63 (2) na (3) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  mamlaka ya bunge ni kutunga sheria na kusimamia serikali. Kutokana na  mamlaka hayo kazi za mbunge ni kuwakilisha wananchi, kushiriki katika  kutunga sheria pamoja na kuisimamia serikali na viongozi wake.
 
 John Mnyika (Mb)
 11/01/2012