BARAZA Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) limemvua uanachama Mbunge wa Wawi na Mjumbe wa Baraza Kuu la chama hicho, Hamad Rashid Mohamed, kwa madai ya kukiuka utaratibu wa chama na hivyo kupoteza sifa za uanachama.
Akitangaza uamuzi huo katika Hoteli ya Manson Mji Mkongwe jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro alisema mbali na Hamad Rashid, pia baraza hilo limewavua uanachama wajumbe wengine watatu wa Baraza Kuu.
Wajumbe hao ni Doyo Hassan Doyo kutoka katika Mkoa wa Tanga, Juma Sanani ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi na Shoka Khamis Juma, aliyewahi kuwa Mbunge wa Micheweni kwa tiketi ya CUF.
"Baraza Kuu la CUF limewafukuza viongozi hao baada ya kuungwa mkono na theluthi mbili kutoka wajumbe wa Tanzania Bara na theluthi mbili kutoka wajumbe Zanzibar," alisema
Mtatiro.
Mjumbe mwingine: Yasin Mrotwa amepewa onyo kali na karipio huku na kwa mujibu wa Mtatiro, anaendelea kuchunguzwa na Baraza Kuu.
Seif dikteta!
Baada ya kuvuliwa uanachama, Hamad Rashid alizungumza na waandishi wa habari na kumuita Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, dikteta na kiongozi asiyeheshimu uamuzi wa Mahakama.
"Sisi tumeweka pingamizi Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa mkutano wa Baraza Kuu na hati ya Mahakama ipo wanayo...sasa nawashangaa wanakiuka sijui kwa nini?" Alihoji Hamad Rashid.
Alisema watakwenda tena mahakamani Februari 14 kusikiliza shauri lao la pingamizi la kikao hicho.
Wengine boya fuata upepo
Alipoulizwa kama anakubaliana na uamuzi wa kikao hicho, alisema anapinga kwa sababu CUF kwa muda wote imekuwa ikiongozwa na Maalim Seif tu; ndiyo mwenye uamuzi na waliobakia wanafuata upepo.
"CUF ni Maalim Seif tu...waliobakia wote ni boya hawana uamuzi wa aina yoyote ndio maana
chama chetu kinaitwa CCM B kwa sababu kinakwenda kinyume na mwelekeo uliokuwepo awali.
UCCM B na Umakamu wa Rais!
"Chama kinafuata sera za CCM si unaona hata Maalim Seif sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais yumo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa," alisema Hamad.
Mtatiro alipoulizwa kuhusu kupokea hati ya mahakama alisema hawaitambui kwani inaweza
kuandikwa na mtu yeyote yule.
Maalim ni Bwana Mkubwa
Naye Shoka alisema CUF sasa inaelekea kubaya kwa sababu imekuwa na uamuzi ya upande mmoja tu kutoka kwa Bwana Mkubwa Maalim Seif.
'Chama sasa kinaelekea kubaya...maamuzi yote ya chama yanatoka kwa Maalim Seif tu....mimi
nimemwambia kwamba amezoea kuwafukuza wanachama wenzake na iko siku atafukuzwa yeye," alisema Shoka.
Alipoulizwa kama atahama CUF au atabaki kuwa muumini wake, alijibu kwamba ataangalia mustakabali wa baadaye.
Yalipoanzia
Mtafaruku ndani ya chama hicho ulianza pale Hamad Rashid, alipoulaumu uongozi na mwenendo wa chama hicho, akisema kuwa Maalim Seif inafaa aache dhamana ya
ukatibu mkuu wa chama.
Duru za wachambuzi wa mambo zilimtuhumu Hamad Rashid kwamba anafanya kampeni ya kuwashawishi wanachama wa CUF wamchague yeye kuwa Katibu Mkuu.
Hatua hiyo ilisababisha Kamati ya Nidhamu ya Chama hicho kuamua kuwahoji Hamad Rashid na wenzake 12 kutokana na tuhuma za kukiuka Katiba ya chama.
Mbunge huyo na wenzake hao ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa na viongozi wa wilaya walitarajiwa kuhojiwa na Kamati hiyo kwa siku mbili mfululizo kutokana na tuhuma kwamba Hamad Rashid na wenzake wanataka kuendesha uasi kwa kumwondoa madarakani
Maalim Seif.
Mbali na Hamad Rashid, wajumbe wa baraza hilo walioingia kwenye tuhuma hizo ni Juma Saidi
Saanani wa Unguja, Shoka wa Pemba, Doyo Hassan Doyo wa Tanga na Yasini Mrotwa wa Mbeya.
Wengine ni Mwenyekiti wa Wilaya ya Ilala, Doni Waziri, Katibu wa Chama hicho wilayani humo, Mohamed Massaga, Mwenyekiti wa Wilaya ya Temeke, Amir Kilungi na Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama katika Wilaya hiyo Mbungilo.
Pia kamati hiyo ilipanga kuwahoji Mwenyekiti wa CUF wa Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi, Nanjase Nanjase; Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mkunduge kata ya Tandale
wilayani Kinondoni, Tamimu Omari na Ahmed Issah wa wilaya ya Morogoro Mjini.
CUF iliamua kuhoji viongozi hao kwa lengo la kujenga mustakabali mwema wa chama hicho baada ya kuibuka malumbano baina ya viongozi wake.
Hata hivyo, Hamad Rashid, aligoma kuhojiwa na Kamati hiyo, akidai kuwa wajumbe watano kati ya wanane wanaoiunda hawakuwa na sifa.
Alisema utaratibu uliotumika kuwateua, haukuzingatia kanuni na taratibu, hivyo hakuwa tayari kuhojiwa na Kamati hiyo na hivyo ikaamua kulipeleka suala hilo Baraza Kuu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Hamad Rashid alitanabaisha kuwa migongano ndani ya CUF, inatokana na majungu yaliyokithiri humo, hivyo ni wazi kwamba hakifanyi kazi kama taasisi.
CHANZO: HABARILEO