Sunday, September 11, 2011

RAMBIRAMBI: MSIBA WA KITAIFA (KUZAMA KWA SPICE ISLANDER)

...Ni habari za kutisha; na zinasikitisha! Hata hivyo, ndiyo mwisho wa ubinadamu - KIFO! Hatuna budi kwanza kushukuru kwa kusema, "SISI NI WA MWENYEZI MUNGU NA KWAKE TUTAREJEA" na "BWANA AMETOA NA AMETWAA; JINA LAKE LIHIMIDIWE" kama desturi yetu. Hata hivyo, kwa nini ajali za mara kwa mara? Hili ni suala la kujiuliza kwa kila mmoja wetu.
 
Wapo wanaodai, "ajali haina kinga"! Inaweza ikachukuliwa kama ni kawaida juu ya dhana hii; na tunaweza kukubali matokeo ya uzembe wetu kuwa ni "kazi ya Mungu; haina makosa"...hapana! Hapa napinga...Mwenyezi Mungu hawezi kusingiziwa uzembe na tamaa zetu za kihayawani.., siyo? Hapana!
 
Upo uzembe wa makusudi unaofanywa na watu wenye roho mbaya na uroho wa kuvuna kutokana na gharama ya binadamu wasiyokuwa na hatia! Vyombo vya usafiri wakati fulani hujaza kupita kiasi na hata mashine na au mitambo yake kushindwa kuhimili uzito na kuzima mara kwa mara vikiwa baharini (kwenye maji). Na magari (mabasi) nayo kadhalika ukiachilia mbali kujaza abiria hali inayozweza kudhinitiwa na Traffic Police; kuna uchakachuaji wa matairi (retreading) na utumizi wa madereva wasiyokuwa na sifa za udereva na hata walevi wa pombe, dawa za kulevya (mirungi) na bangi!
 
Tamaa ya kupata faida ya mali imewashika wenye vyombo vya usafiri na hata kupelekea kutojali usalama wa abiria kwa gharama ya maisha ya watu mali zao! Hali hii inatisha na inasikitisha sana. Tuna kila sababu ya kujipanga na kuzuia ajali zinazoepukika kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa vyombo vya usafiri wa majini na nchi kavu. Kinyume chake ajali zitaendelea kulisakama taifa na kupoteza nguvukazi kubwa na hasara ya mali pia.
 
Mungu (Mwenye Enzi) Awalaze mahala penye stahili zao marehemu wetu wote na Awape nafuu na akhueni ya haraka manusura wote, amina! Mungu Ibariki Tanzania; Wabariki na Wananchi wa Tanzania...
 
Amani ya Mwenyezi Mungu iwe kwenu nyote!

Mdau Kutoka Tanzania