Friday, June 10, 2011

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI-Kuhusu Bajeti ya serikali (Mh. Zitto Kabwe)

OFISI YA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

"Hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/2012 ina upotoshaji
mkubwa"

Kutokana na Hotuba ya bajeti ya Waziri wa Fedha, Mhe. Mustafa Mkullo
(Mb), aliyoitoa jana bungeni Dodoma tarehe 08/06/2011, kuhusu makadirio
ya mapato na matumizi ya serikali kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa
2011/2012. Kambi ya Upinzani tumeshtushwa na upotoshaji mkubwa wa
kitakwimu na kimaudhui uliofanywa na serikali kwa lengo la kuwajengea
matumaini hewa wananchi kuwa watapata nafuu ya maisha kupitia bajeti
hiyo wakati hali halisi haipo hivyo.

Yafuatayo ni baadhi tu ya maeneo ya waziwazi ambayo serikali ya CCM
kupitia kwa Waziri wake Mhe. Mkulo iliamua kuupotosha umma wa
Watanzania kwa makusudi kama ifuatavyo;

1. Wakati Waziri akitaja kuwa kipaumbele cha kwanza cha bajeti hiyo ni
kumaliza tatizo la Umeme na hivyo kutamka kwamba ametenga shilingi
537 Bilioni, , upembuzi uliofanywa na Kambi yetu ya Upinzani kwenye
vitabu vya bajeti (Kitabu Namba II na IV) vilivyotolewa na serikali
yenyewe, umebaini kuwa Wizara ya Nishati na Madini imetengewa
jumla ya kiasi cha shilingi 402,402,071,000 milioni kwa mujibu wa
fungu la 58. Fedha hizo zimegawanywa katika mafungu ya Matumizi
kawaida shilingi 76,953,934,000 milioni na kwa upande wa bajeti ya
Maendeleo zimetengwa shilingi 325,448,137,000. Shilingi Bilioni 325
zilizotengwa katika Bajeti ya Maendeleo ya Wizara ya Nishati na Madini
zinatosha kwa mradi mmoja tu wa umeme wa 160MW, 100 Dar es
Salaam na 60 Mwanza. Hakuna mradi wowote mpya wa umeme
unaonekana katika Bajeti. Ni dhahiri kuwa kauli ya Mkulo ililenga zaidi
kuwajengea wananchi matumaini hewa kuliko kuchukua hatua za kweli
za kumaliza tatizo la umeme.

2. Wakati Waziri na Serikali wanataka kuwaaminisha Watanzania kuwa
bajeti ya mwaka huu imeongezeka kuliko ilivyokuwa mwaka 2010/2011,
ukweli ni kuwa hakuna ongezeko halisia (real term increase) lililofanyika.
Bajeti iliyopita ilikuwa kiasi cha shilingi 11.6 trilioni wakati mwaka huu wa
2011/2012 serikali ina bajeti ya jumla ya shilingi 13.525 trilioni. Kati ya
ya fedha hizo za mwaka 2011/2012, kiasi cha shilingi 1.901 trilioni
ambazo ni sawa na asilimia 14.06% ya bajeti yote, kitatumika kulipia
deni la Taifa. Kwa mantiki hiyo, mtaona kuwa fedha kwa ajili ya
kuendesha serikali pamoja na kugharamia miradi mbalimbali ya
maendeleo zitabaki kuwa ni kiasi cha shilingi trilioni 11.624 ambazo ni
sawa na fedha za bajeti ya mwaka uliomalizika wa 2010/2011 (Japo
thamani ya shilingi imeanguka ukilinganisha na hali ilivyokuwa mwaka
2010/2011). Tunasisitiza kuwa hii si bajeti ya maendeleo, hii ni
bajeti ya madeni.
3. Wakati Waziri akisema Bungeni kuwa Bajeti ya mwaka 2011/2012
itapunguza posho kama sehemu ya mkakati wa serikali wa kuthibiti
matumizi, nanukuu "kupunguza malipo ya posho mbalimbali
yasiyokuwa na tija (uk.53)", ukweli ni kuwa Bajeti ya serikali ya mwaka
2011/2012 imetenga jumla ya shilingi 0.987 trilioni ambazo ni sawa na
asilimia 13 % ya recurrent budget ya serikali kwa ajili ya kulipa posho
chini ya vifungu vinavyojulikana kama "Personnel allowances (non
discretionary na In-kind"). Kwa hiyo, kauli ya Waziri Mkulo kuwa
serikali itapunguza posho sio kweli. Tunautaka umma wa
Watanzania usikubali kurubuniwa.

4. Wakati Waziri akisema kuwa ili kuthibiti matumizi watapunguza posho
mbalimbali, kwenye hotuba yake uk.66, waziri amependekeza
kufanywa kwa marekebisho ya sheria ya kodi ya mapato SURA 332 na
anasema kwenye (i) "kusamehe kodi ya mapato kwenye posho
wanazolipwa wafanyakazi wa serikali na wanaofanya kazi kwenye
taasisi zinazopata ruzuku kutoka kwenye bajeti ya serikali" . Hii
inaonyesha dhahiri kuwa kauli ya Kufuta au kupunguza posho ilitolewa
na Serikali ili kupumbaza wananchi lakini haina udhati.

5. Bajeti ya serikali ya mwaka 2011/2012 imewaongezea mzigo mkubwa
sana wananchi na haswa wajasiriamali wadogo na vijana ambao
wamejiajiri ama kuajiriwa kwenye biashara ya usafiri na usafirishaji.
Tunasema hivyo, kwa sababu serikali katika bajeti vyake rasmi vya
bajeti imeamua kufanya marekebisho ya sheria ya usalama barabarani
sura 168 ili kuongeza ukomo wa kiwango cha faini inayotozwa kwa
kufanya makosa wakati mtu akiwa anaendesha gari yaani (Traffic
Notification Fee), kutoka shilingi 20,000 hadi shilingi 300,000. Lakini

Waziri Mkulo katika Hotuba yake aliyoitoa jana ukurasa 74, alitamka
kuwa wataongeza kiwango cha faini hadi kufikia shilingi 50,000. Ni
dhahiri kuwa kauli ya waziri ya kusema faini itafikia 50,000 wakati
kwenye vitabu rasmi vya bajeti faini hiyo inaonekana itafikia 300,000,
hivyo alilenga kuuhadaa umma na kuupotosha.

6. Kambi ya Upinzani Bungeni imeshtushwa na kushangazwa na
hatua ya Serikali kutenga zaidi ya robo ya Bajeti kulipa Madeni na
Kulipana Posho (Asilimia 27 – 14% kulipa madeni na 13% kulipa
Posho mbalimbali).
7. Kambi ya Upinzani itawasilisha Bungeni Bajeti Mbadala siku ya
Jumatano tarehe 15.6.2011, saa tano asubuhi ambayo itakuwa inajali
masilahi ya Watanzania yenye lengo la kukuza Uchumi wa Vijijini
(rural growth) na itajikita katika kupata vyanzo vipya vya mapato na
kubana matumizi ikiwemo kufuta Posho mbalimbali.
Imetolewa leo, Mjini Dodoma, na

Zitto Zuberi Kabwe

Waziri Kivuli wa Fedha
Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni