Shule za Serikali zapeta Kidato cha Sita
Thursday, 28 April 2011 21:16
0diggsdigg
Fedelis Butahe
SHULE za Sekondari za Serikali zimeng’ara katika matokeo ya Kidato cha sita mwaka 2011 baada ya wanafunzi wake saba kuwa miongoni mwa wanafunzi kumi bora kitaifa.Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa jana jijini Dar es Salaam, wanafunzi kumi waliofanya vizuri zaidi kitaifa ni wavulana.Akitangaza matokeo hayo Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), Dk Joyce Ndalichako aliwataja wanafunzi kuwa ni Muhagachi Chacha (Kibaha), Samwel Katwale, George Felix (Mzumbe), Amiri Abdalah, Comman Nduru na Kudra Baruti (Feza Boys), Aron Gerson, Shaban Omary na Francis Josephat (Tabora Boys), George Assenga (Majengo).
Wasichana waliofanya vizuri
Dk Ndalichako pia aliwataja wasichana kumi waliofanya vizuri zaidi katika mtihani huo na shule zao kwenye mabano kuwa ni Doreen Kabuche (Benjamin Mkapa), Rahabu Mang’amba (Kilakala), Mary Mosi (Kifungilo Girls), Nuru Kipato (Marian Girls), Zainabu Hassan (Al-Muntazil Islamic), Catherine Temu (Ashira).
Wengine ni, Anthonia Lugomo (Usongwe), Cecilia Mville (Kifungilo Girls), Mariam Matovola (Kilakala) na Suzana Makoi (Tarakea).Dk Ndalichako alisema wanafunzi 59,112 waliandikishwa kufanya mtihani huo, wakiwamo wasichana 21,291 na wavulana 37,821, lakini watahiniwa 1,966, hawakufanya mtihani.
Alitaja shule kumi bora katika kundi la shule zenye watahiniwa zaidi ya 30 kuwa ni, Marian Girls, Feza Boys, Kifungilo, Kibaha, St Mary’s Mazinde, Ilboru, Tabora Boys, St Mary Goreti, Mzumbe na Mafinga Seminari.
"Shule kumi bora zenye watahiniwa chini ya 30 ni Uru Seminary, St James Seminary, Maua Seminary, Same Seminary, Dungunyi Seminary, DCT Jubilee, Parane, St Joseph- Kilocha Seminary, Mlama na Masama Girls,"alisema.
Dk Joyce Ndalichako alisema watahiniwa 49,653 waliofanya mtihani huo Februari mwaka huu, wamefaulu.
"Kati yao wasichana ni 18,351 (sawa na asilimia 88.74) na wavulana ni 31,302 (sawa na asilimia 86.38) na kuongeza kuwa mwaka 2010 watahiniwa waliofaulu walikuwa 55,772 sawa na asilimia 88.85,"alisema na kuongeza:
Watahiniwa waliosajiliwa
“Kati ya watahiniwa wa shule 44,958 waliosajiliwa, watahiniwa 44,720 ndio waliofanya mtihani huo, wasichana walikuwa 16,327 na wavulana walikuwa 28,393, watahiniwa 23 hawakufanya mtihani,” alisema Ndalichako,
Aliongeza: “Watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa walikuwa 14,154, waliofanya mtihani walikuwa watahiniwa 12,426 na watahiniwa 1,728 hawakufanya mtihani.”
Alifafanua kuwa mwaka huu watahiniwa wa shule waliofaulu ni 40,960 sawa na asilimia 92.03 ya watahiniwa wote waliofanya mtihani. Kati yao wasichana walikuwa 15,088 sawa na asilimia 92.63 na wavulana ni 25,872 sawa na asilimia 91.69.
"Idadi hiyo ni tofauti na ya mwaka 2010 ambapo watahiniwa wa shule 45,225 sawa na asilimia 93.76 ndio waliofaulu mtihani huo," alisema.
Alisema kuwa watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani huo ni 8,693 sawa na asilimia 70.05. "Mwaka 2010 watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani huo walikuwa 10,547 sawa na asilimia 72.57," alieleza.
Ubora wa ufaulu
Akizungumzia ubora wa ufaulu, Ndalichako alisema kuwa watahiniwa 34, 949 ambao ni jumla ya wasichana 12,868 na wavulana 22,081, wamefaulu katika daraja la I-III.Alisema kuwa watahiniwa wa shule walifanya vizuri katika masomo ya Hisabati, Jiografia, Fizikia, Kemia, Uchumi na Biashara ikilinganishwa na mwaka jana.
Katika hatua nyingine, Dk Ndalichako alisema kuwa Necta imesitisha matokeo ya mtihani huo kwa watahiniwa 218 kwa kuwa hawakulipa ada ya mtihani na kwamba yatatolewa mara baada ya kulipa ada hiyo.“Necta pia imefuta matokeo yote ya watahiniwa watano wa shule na watahiniwa sita wa kujitegemea waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani,”alisema Ndalichako.
Source: Mwananchi