Tuesday, October 19, 2010

Wasiosajili simu kuburuzwa kortini



Tuesday, 19 October 2010 08:11
Salome Kuga na Emmy Kihongole
WATUMIAJI huduma za simu za mikononi wapatao milioni nne watafikishwa mahakamani ambako wanaweza kuhukumiwa kifungo au faini kutokana na kushindwa kusajili laini zao kabla ya Oktoba 15.
Mkurugenzi msaidizi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Richard Kayombo aliliambia gazeti hili jana kuwa mbali na adhabu hiyo, simu hizo zitafungiwa.

“Sheria mpya ya mawasiliano imeanza kutumika kuanzia Mei 15 mwaka huu na mtu yoyote ambaye hajasajili laini yake, atakumbana na adhabu zilizoainishwa katika sheria hiyo," alisema Kayombo.
“Kesho (leo) tutakutana na kampuni zote za simu katika kikao ambacho kitajadili agenda mbalimbali, ikiwemo hii ya simu hizo na adhabu wanazopaswa kupewa wahusika."

Hata hivyo, Kayombo hakubainisha njia watakazotumia kuwanasa wasiosajili simu na kuwapeleka mahakamani.
Kwa mujibu wa Kayombo usajili wa simu ulioanza mwezi Juni mwaka jana, ulimalizika Oktoba 15 mwaka huu na yeyote ambaye alikuwa hajasajili simu yake, atakuwa ametenda kosa kisheria.
Kayombo alieleza kuwa hadi Oktoba 15 mwaka huu, laini milioni 16 za simu, ambazo ni asilimia 76 ya watumiaji milioni 20 wa simu zote, zilisajiliwa.

Kayombo alisema kadi zote zinazouzwa kwa sasa zinatakiwa zisajiliwe kwanza na kuzitaka kampuni za simu za mkononi kuwapiga marufuku mawakala wake wanaouza kadi hizo bila kuzisajili.

Pia alizitaka kampuni zote za simu kuwa makini na mawakala wao ambao wanaouza laini bila ya kusajili, akiyataka yaamuru waache mara moja kwa kuwa wakibainika sheria itafuata mkondo wake.
Katika hatua nyingine, Kayombo alitoa wito kwa watumiaji wote  wa simu za mkononi, kutumia vizuri simu zao bila kuwabugudhi watu wengine.
“Sheria zipo wazi kwa hiyo mtu atakayebainika kutumia simu yake vibaya kwa kutukana watu au mambo mengine kama hayo, atachukuliwa hatua,” alieleza.

Source Mwananchi.