Mahakama yatupa kesi dhidi ya Kikwete | |
Tuesday, 19 October 2010 08:18 |
James Magai MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali kesi iliyofunguliwa na Mwalimu wa zamani, Paul John Mhozya, akipinga hatua ya Rais Jakaya Kikwete kugombea kwa mara ya nyingine kiti cha urais, katika uchaguzi mkuu mwaka huu. Mhoza alifungua kesi hiyo Julai 22 chini ya hati ya dharura akiiomba mahakama hiyo iiamuru Tume ya Uchaguzi ya Taifa, imuondoe Kikwete katika orodha ya wagombea wa urais. Katika hati yake ya madai, pamoja na mambo mengine Mhozya alidai kuwa Kikwete hastahili kugombea tena nafasi hiyo kwa madai kuwa katika kipindi chake cha kwanza cha urais, amevunja haki za binadamu. Pia alidai kuwa katika kipindi chake cha kwanza cha urais amekuwa na safari nyingi za nje, akitumia pesa kutoka Hazina kwa ajili ya starehe zake binafsi, huku akiwadanganya Watanzania kuwa safari hizo zimekuwa na manufaa kwao. Akitoa uamuzi dhidi ya pingamizi lililowekwa na upande wa mlalamikiwa wa kwanza ambaye ni Bodi ya Wadhamini wa Chama Cha Mapinduzi, kilichomteua Kikwete kugombe tena nafasi hiyo na mlalamikiwa wa pili (Tume), Jaji Agustine Shangwa alisema madai ya mlalamikaji hayana msingi. Katika uamuzi wake huo Jaji Shangwa, alikubaliana na hoja mbalimbali za pingamizi zilizowasilishwa na wakili wa serikali, Abrahamu Senguji kwa niaba ya mlalamikiwa wa pili na wakili Sam Mapande kwa niaba ya mlalamikiwa wa pili . Akisisitiza kuunga mkono hoja za pingamizi, Jaji Shangwa alisema katika hati ya madai ya mlalamikaji hakuna kitu chochote kinachoonyesha kuwa kama kuna haki na wajibu wake wowote ulioainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambazo zimekikwa na mgombea huyo wa CCM. "Kwa hiyo ni maoni yangu kwamba madai yaliyofunguliwa na Paul John Mhozya, hayana nguvu si tu kwa kutodondoa kipengele rasmi cha sheria ambayo ameitumia kufungua madai yake yaani sheria ya ukaziaji wa haki na wajibu wa msingi, lakini pia kwa kuleta maombi hayo chini ya sheria ambayo haitumiki katika kumuengua mgombea yeyote katika kushiriki kinyang'anyiro cha urais katika nchi hii,"”alisema Jaji Shangwa. Jaji Shangwa alisema kwa msingi huo hakuna tena haja ya kuendelea kuangalia hoja nyingine ya pingamizi iliyowasilishwa na upande wa mlalamikiwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kisheria kusikiliza shauri hilo. Jaji Shangwa pia alikubaliana na hoja za pingamizi zilizowasilishwa na mawakili wa walalamikiwa wote kuwa madai ya mlalamikaji hayana msingi na kwamba yaliyomo katika madai hayo tuhuma za kiujanja za kipropaganda. Alipinga madai na tuhuma za mlalamikaji akidai kuwa Kikwete ambaye aliteuliwa na chama chake kuwa mgombe bila, mpinzani anastahili kuwa mgombe katika uchaguzi mkuu mwaka huu. Kuhusu madai ya safari za nje, Jaji Shangwa alisema kuwa safari hizo hazikuwa kwa manufaa yake binafsi kama mlalamikaji alivyodai kuwa zilikuwa ni za kiofisi. Pia alisema kuwa kwa muda ambao amekuwa katika uongozi Kikwete ameweza kujenga uhusiano mzuri na wananchi wote na kwamba ameweza kudumisha uhusiano mzuri kati ya Tanzania na nchi n yingine jirani na Afrika kwa jumla. Jaji Shangwa pia alisema Kikwete amedumisha sera ya kutofungamana na nchi yoyote zenye nguvu za kijeshi na kiuchumi kama vile Marekani, Urusi na China. Lakini pia Jaji Shangwa alisema katika kipindi ambacho amekuwa madarakani hakuna tangazo au taarifa yoyote rasmi kuwa ametenda kosa lolote kuhusiana na matumizi mabaya ya madaraka yan kiofisi. |