Monday, October 25, 2010

Maswa hapakaliki, MGOMBEA WA CCM NAYE AMFUATA SHIBUDA LUPANGO

Maswa hapakaliki, MGOMBEA WA CCM NAYE AMFUATA SHIBUDA LUPANGO  
Monday, 25 October 2010 07:20  

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba
Zulfa Mfinanga, Shinyanga na Frederick Katulanda, Mwanza
HALI inaonekana kuwa tete kwenye Jimbo la Maswa Magharibi baada ya mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Robert Kisena kukamatwa na kuwekwa mahabusu, siku chache baada ya mgombea wa Chadema, John Shibuda kukamatwa kwa tuhuma za kuhusika kwenye vurugu zilizosababisha kifo cha dereva wa CCM.

Shibuda, ambaye ameliongoza jimbo hilo kwa tiketi ya CCM kwa kipindi kirefu kabla ya kuhamia Chadema, alikamatwa wiki iliyopita baada ya wafuasi wa chama hicho kupambana na wenzao wa CCM karibu na eneo ambalo Chadema ilikuwa ikiendesha mkutano wake wa kampeni za ubunge, vurugu zilizosababisha Steven Kwilasa Masanja, 26, ambaye alikuwa akimuendesha Kisena, kupoteza maisha.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Shinyanga, Daudi Siasi alithibitisha kukamatwa kwa mgombea ubunge huyo wa CCM, ambaye vyombo vya habari viliripoti kuwa siku ya vurugu hizo alikwenda kituo cha polisi na kumshambulia kamanda wa polisi wa wilaya na kumbwaga chini, akimtuhumu kuwa alimwachia huru Shibuda.

Kukamatwa kwa Kisena kumekuja siku moja tangu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba 'kuweka kambi' wilayani Maswa mkoani Shiyanga kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo la kwanza la aina yake kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Wakati Manumba akiwa wilayani Maswa kuratibu uchunguzi wa mauaji hayo, katibu mkuu wa CCM, Yusuph Makamba tayari ameshakaririwa na vyombo vya habari akidai kuwa chama chake kina ushahidi wa kimazingira kuwa mgombea huyo wa Chadema alihusika na mauaji hayo ya dereva wa mgombea wa CCM.

Habari za kipolisi zinasema kuwa Kisena alitiwa nguvuni na polisi jana akihusishwa pia kwenye tukio hilo, lakini taarifa zaidi zinadai kuwa mgombea huyo wa CCM alikamatwa pia kwa tuhuma za kumshambulia kwa mateke kamanda wa polisi wa Wilaya ya Maswa (OCD), Peter Ndunguru.

"Mgombea huyo (Kisena) ametiwa nguvuni kutokana na mzozo wake na OCD wa Maswa juzi kituoni hapo na kumpiga OCD," alisema Kamanda Siasi, ambaye mwishoni mwa wiki alikaririwa akisema kuwa suala la shambulizi hilo ni la OCD Ndunguru na si Jeshi la Polisi na kufafanua kuwa ofisa wake ndiye aliyetakiwa kuamua au kutoamua kumshtaki mgombea huyo kwa tuhuma hizo za kufanya jinai.

Akizungumza kwa njia ya simu siku ya tukio, OCD Ndunguru alisema mgombea huyo wa CCM aliyeambatana na viongozi wa chama hicho walifikika polisi na kuuliza mahali alipo Shibuda, lakini kabla ya kujibiwa Kisena alimrukia OCD na kuanza kumshambulia kwa mateke kiasi cha kumuangusha chini.

“Alinirukia na kunipiga,” alieleza OCD, lakini 'bosi' wake, ambaye ni Kamanda Siasi, akasema kuwa “Suala la Kisena na OCD ni jambo la kawaida kiutendaji na wala siwezi kulizungumzia... kwa sasa hapa ninashughulika na suala zito la mauaji".

Taarifa zaidi zinasema tayari Jeshi la Polisi limeunda tume ya watu wanne kuchunguza vurugu hizo baina ya wafuasi wa Chadema na CCM ikiongozwa na DCI  Manumba ambaye yupo Maswa kuchunguza chanzo cha vurugu hizo zilizosababisha Shibuda kuwekwa rumande hadi leo.

Taarifa zinasema katika timu hiyo ya uchunguzi, Manumba ameongozana na mmoja wa maafisa waaandamizi wa upelelezi makao makuu ya polisi Dar es Salaam na watashirikiana na mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Shinyanga, Selemani Nyakipande, pamoja na maafisa Idara ya Usalama wa Taifa ambao hata hivyo hawajatajwa.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu juzi, Manumba alisema kuwa amefika kwa ajili ya kusaidia safu ya uchunguzi ili kuhakikisha haki inatendeka na ukweli unabainika.

“Ndiyo niko Maswa, lakini ndiyo tumeanza uchunguzi... naomba nipewe nafasi ya kufanya kazi; tukikamilisha uchunguzi wetu juu ya jambo hili tutawafahamisheni,” alieleza Manumba.

Jana Manumba alisema ni mapema mno kuzungumzia tume hiyo na akakiri kuwa yeye ni mmoja wa wajumbe akiongeza kuwa Shibuda na wenzake bado wanashikiliwa na polisi.

"Sijaunda tume kwa kuwa hata mimi mwenyewe ni mmoja wa watu walio kwenye tume hiyo ndiyo maana nikaja hapa, lakini siwezi kuzungumzia kwa sasa hadi tutakapomaliza kazi; lakini Shibuda bado yupo ndani," alisema Manumba.

Shibuda pamoja na watuhumiwa wengine 12 alikamatwa Oktoba 21 majira ya saa 10:00 jioni wakituhumiwa kuhusika na tukio la mauaji ya dereva wa gari la mgombea ubunge wa CCM, Robert Simon Kisena katika Kijiji cha Kizungu.

Taarifa zaidi zinasema kuwa marehemu Kwilasa aliyezaliwa mwaka 1984, amezikwa jana kijijini kwao Badabada, Kata ya Nyalikungu na mazishi yake yalihudhuriwa na mkuu wa mkoa Shinyanga, Dk Yohana Balele, mwenyekiti wa CCM mkoa huo, John Mgeja na katibu wake, mgombea ubunge, Teddy Kasela Bantu na Ridhwani Kikwete.

Hata hivyo, taarifa zilizolifikia gazeti hili wakati tukienda mitamboni zinaeleza kuwa Kisena alionekana kwenye mazishi hayo ya aliyekuwa dereva wake huku polisi wakidai kumuachia huru kwa dhamana baada ya kuhojiwa.

"Ameachiwa kwa dhamana. Tulimkamata; tukamhoji... dhamana ilikuwa wazi na ametimiza masharti," alisema mkuu wa upelelezi mkoa huo (RCO), Seleman Nyakipande.

Hata hivyo, Mwananchi ilipotaka kujua sababu za mgombea huyo wa CCM kuachiwa huru mapema tofauti na Shibuda anayeendelea kushikiliwa, Nyakipande alisema "Kisena hawezi kuhusishwa na vurugu zilizotokea kwa sababu alikuwa mbali na tukio."

Mwananchi ilipohoji kuwa mbona taarifa zinaonyesha kuwa hata Shibuda alikuwa mbali na tukio, RCO huyo alisema: "Tulimkamata Shibuda kwa ajili ya uchunguzi na tutamwachia hivi karibuni."

Akiwa wilayani Maswa juzi, Makamba alisema: “Kwanza kabla ya yote Chadema walishatangaza kuwa ni lazima watamwaga damu na katika tukio hili kuna ushahidi wa kimazingira kuwa Shibuda anahusika na mauaji hayo... pia kuna ushahidi wa kimazingira kuwa wafuasi wa Chadema wanahusika na mauaji hayo.”

Vurugu hizo zilitokea Oktoba 21 majira ya saa 10:00 alasiri kwenye eneo lililo mbali na uwanja ambao Shibuda alikuwa akihutubia kijijini Kizungu. Wafuasi wa Chadema waliokuwa wakitangaza kuwepo kwa mkutano huo wa Shibuda kwa kutumia gari la matangazo, walikutana na gari la wafuasi wa CCM wakati wakielekea kwenye mkutano wao na ndipo vurugu kubwa zilipozuka na hatimaye kusababisha kifo.

Kamanda Siasi aliwaambia waandishi kuwa wafuasi wa CCM walipofika eneo hilo waliteremka kwa ajili ya kukojoa na baadaye gari la Chadema lilisimama na wafuasi hao wakaanza kushambuliana.

Kamanda Siasi alisema kuwa mbali na kuuawa kwa dereva huyo, wafuasi wengine wanne wa CCM waliokuwa kwenye gari hilo aina ya Toyota Hilux Surf, walijeruhiwa katika mapambano hayo na kuwataja kuwa ni Msaada Mangulu mwenye umri wa miaka 33, Sita Mashara, 32, Alexernder Edward, 43, pamoja na William Simon, 32, ambaye ni mdogo wa mgombea huyo wa CCM na kwamba hali zao zinaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu na kuruhusiwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Maswa.

Kutokana na vurugu hizo, Shibuda ambaye alikuwa akiendelea na mkutano wake, alifuatwa na maofisa wa polisi na kuwekwa chini ya ulinzi na hadi jana alikuwa akiendelea kushikiliwa kwa mahojiano.

Akizungumzia tukio hilo, Shibuda alisema alidai kuwa kushikiliwa kwake kunatokana na maagizo ya CCM kwa vile wanataka kutumia njia hiyo kummaliza kisiasa licha ya kuwa wanatambua kuwa wakati tukio hilo alikuwa jukwaa akiendelea na kampeni.

Alisema kushikiliwa kwake kunaonyesha ni jinsi gani ambavyo jeshi hilo linatumiwa na CCM kumkandamiza kwa kuwa eneo alilokuwa akihutubia yeye lilikuwa mbali na eneo la tukio, lakini amepata taarifa kutoka kwa baadhi ya maofisa wa polisi kuwa wamepewa maelekezo na vigogo wa juu wa CCM kuwa asiachiwe. Source: Mwananchi