Thursday, September 30, 2010

NEC yasema CHADEMA acheni Uchochezi

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeionya Chadema kuacha kauli zake za kwamba, kuna njama za kuandaa karatasi za kupigakura za kuwezesha ushindi wa Rais Jakaya Kikwete, kwani zikiingia kwa watu wasioweza kuzichambua zinaweza kuleta hatari.

Onyo hilo la NEC linakuja baada ya Chadema kutangaza hadharani kwamba, kitengo chake cha usalama kimebaini njama za kuwepo mpango wa kutengeneza karatasi nje ya nchi ambazo zitasaidia kuchakachua matokeo ili Kikwete awe rais.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa NEC Jaji Lewis Makame, alisema tuhuma hizo ni za uongo na za kutungwa.

Kwa mujibu wa Jaji Makame, kama kungekuwa na mpango kama huo NEC isingeweza kuamua kupeleka karatasi hizo nje ya nchi kwa ajili ya kuchapishwa kwa usalama zaidi.

"Mimi nasema tuhuma  hizo ni za uongo kwani hazina ukweli wowote. Hivi inawezaje kuingia akilini tukafanye mpango kama huo nje ya nchi, si tungeweza kuamua kufanya hapa kwetu?" alihoji  Makame.

Mwenyekiti huyo alifafanua kwamba, kauli kama hizo zinaweza kuwa na hatari kama zitaingia kwenye akili za watu wasiojua kuchambua mambo na kubaini mbivu na mbichi.

"Sisi tutahakikisha Rais anayeshinda ni yule aliyechaguliwa na wananchi tu na si vinginevyo. Hatuwezi kukiuka matakwa ya wananchi," alisisitiza Jaji Makame.

Makame alisisitiza kwamba, kilichofanyika katika kuipata kampuni hiyo iliyopewa zabuni ni kutangazwa zabuni ya wazi kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Jaji Makame alisema kampuni hiyo, iliyopewa dhamana ya kuandaa karatasi hizo, haikuchaguliwa na CCM wala Rais Kikwete.

"Kampuni ilichaguliwa baada ya kufuatwa taratibu zote husika za zabuni, tulitangaza zabuni kwa mujibu wa sheria. Sasa kuanza kusema kuna mpango wa kuharibu matokeo kupitia ballot papers ni uongo mkubwa," alisisitiza.

Alisema NEC imejipanga kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa huru na wa haki huku akisisitiza kwamba, tumekuwa tukituma vijana wetu mara kwa mara kuangalia mchakato huo kwa kampuni husika.

Jaji Makame aliweka bayana kwamba,  hatua hiyo ya kutuma vijana wake mara kwa mara ni kuona kama kazi iliyopangwa kufanywa kwa mujibu wa zabuni, inatekelezwa.

Alisema NEC ina dhamana na uchaguzi mkuu na kwamba mchakato mzima wa kuandaa karatasi za kupigiakura uko chini yao, hivyo kuhusisha taasisi nyingine ni hatari.

Juzi Dk Slaa, akizungumza na waandishi wa habari pasipokutaja nchi yenyewe, alisema wanazo taarifa za siri kutoka kitengo chao cha usalama alichokiita makini, kimebaini mpango huo wa kuchezea kura kupitia karatasi hizo.
 
Chanzo: Mwananchi