Thursday, January 29, 2009

Mradi wa magari yaendayo kasi kujenga barabara za zege Dar

Dar sasa ni Tambarare,

Hebu soma kisa hiki....................

Mradi wa Magari yaendayo kasi jijini Dar es Salaam (DART) unatarajia kuanza kujenga barabara kwa kutumia zege badala ya lami, zitakazotumika kupitisha magari hayo ambapo dola za Marekani milioni 122.1, sawa na Sh. bilioni 150 zinatarajia kutumika. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mtendaji Mkuu wa DART, Cosmas Takule, alisema kutokana na uimara wa barabara hizo za zege, wana uhakika wa kudumu kati ya miaka 20 hadi 30 bila kufanyiwa matengenezo yoyote. Huduma za magari hayo zitaanza Novemba mwakani. Alisema barabara za lami zinadumu kati ya miaka mitano hadi tisa kama hazikufanyiwa matengenezo. Kadhalika, alisema mradi huo utajumuisha ujenzi wa maeneo ya maegesho ya magari jijini Dar es Salaam. Alisema mradi huo utakapokamilika utasaidia kupunguza msongamano wa magari, tatizo ambalo limekuwa sugu hivi sasa jijini Daer es Salaam. Alisema katika awamu ya kwanza ya mradi, watajenga barabara kuanzia Kimara hadi kivukoni jijini Dar es Salaam na kwamba hakuna gari yoyote itakayoruhusiwa kupita hapo zaidi ya magari yaendayo kasi. Alifafanua kuwa barabara hiyo itakuwa na vituo vitano kutoka mwanzo hadi mwisho. Takule alisema hawatatenga eneo jipya la kujenga barabara hizo bali zitakuwa sambamba na ile ya Morogoro inayotoka Kimara hadi kati kati ya jiji la Dar es Salaam. Aidha, baadhi ya barabara zitaongezwa na kufanywa ziwe za kwenda bila magari kupishana (oneway). Aidha, alisema wataweka barabAra za juu katika makutano ya barabra za Mandela, Sam Nujoma na ile ya Nyerere. Takule aliwataka wananchi kuamimini kwamba mradi huo upo na tayari serikali imetoa Sh. bilioni 10 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi watakaobomolewa nyumba zao zilizopo kando kando mwa zitakapopita barabara hizo. Kwa upande mwingine alisema kutakuwa na magari ya mzunguko kuanzia eneo la Wazo, Kunduchi, Mwenge, Tabata, Uwanja wa Ndege, Mbagala na kuishia Kigamboni jijini Dar es Salaam. Kuhusu mkandarasi alisema, DART ipo katika mchakato wa kumtafuta na kwamba mara baada ya kumpata, ujenzi utaanza muda wowote.
SOURCE: Nipashe