Thursday, January 26, 2017

WAZIRI JAFO AWASHANGAA WANASHERIA WA HALMASHAURI KUSHINDWA KESI


WAZIRI JAFO AWASHANGAA WANASHERIA WA HALMASHAURI KUSHINDWA KESI

Naibu Waziri wa Nchi TAMISEMI Mhe. Suleimani Jafo (Mb) akitoa hotuba katika kikao cha kazi katika ukumbi wa mikutano Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini mjini Dodoma akiwaasa wanasheria kuhakikisha sheria ndogo hazikinzani na sheria mama kwa kuzingatia uandishi wa taaluma ya sheria kwani katika baadhi ya ziara zake amebaini kuwepo mogogoro ya wakulima na wafugaji, kesi nyingi za halmashauri kushindwa mahakamani na uandishi mbovu wa mikataba inayoingia halmashauri
Naibu Waziri wa Nchi TAMISEMI Mhe. Suleimani Jafo (Mb) akisisitiza jambo kuhusu uendeshaji wa vikao vya Halmashauri kwamba Madiwani wanapaswa kuelekezwa kanuni na sheria za Halmashauri ili kuepuka migogoro ambayo mingi inaibukia wakati wa vikao vya mabaraza katika Mamlaka hizo. Kushoto kwake ni Sarah Barahomoka (Mwandishi Mkuu wa sheria bungeni) na Mwanasheria wa Idara ya Sheria OR TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu OR TAMISEMI Bw. Benard Makali akisisitiza jambo juu ya makosa yanayofanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kama ukiukwaji wa utendaji kazi wa kisheria ambapo wanasheria wanapaswa kusimamia masuala yote ya kisheria katika utendaji wa kazi za Serikali
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu (Shinyanga) ambaye pia ni Mwanasheria Bw. Stephen M.Magoiga akimshukuru Naibu Waziri OR TAMISEMI Mhe. Suleimani Jafo (Mb) kwa niaba ya Wanasheria ambapo amewaasa Wanasheria wenzake kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuzifanyia kazi sheria ndogo kwa ustawi wa Mamlaka za Serikali nchini.
Baadhi ya Wanasheria wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nchi TAMISEMI Mhe. Suleimani Jafo (Mb) wakati akitoa hotuba katika kikao cha kazi katika ukumbi wa mikutano Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini mjini Dodoma ambapo amewaasa kufanya kazi kwa bidii na umuhimu wa sheria ndogo katika uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

…………….

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo, amefungua mafunzo ya siku tatu ya wanasheria kwenye Halmashauri zote nchini huku akioneshwa kukerwa na tabia ya wanasheria hao kushindwa kesi na kuisababishia hasara serikali kwa kuwalipa fidia washindi.

Akifungua mafunzo hay oleo mkoani Dodoma, Jafo amesema zipo kesi nyingi zinazohusu halmashauri mbalimbali, lakini zinashindwa kutetewa na kusababisha serikali kulipa fidia.

Amebainisha pamoja na kuwepo wanasheria ndani ya halmashauri hizo, lakini wanashindwa kusimamia kesi zinazowakabili hali inayochangia serikali kulipa gharama kubwa kwa washindi wakati fedha hizo zingetumika kwa maendeleo ya wananchi.

"Fedha zinazolipwa na serikali mara baada ya kushindwa kesi, zingeweza kusaidia maendeleo ya wananchi ndani ya halmashauri hizi kutokana na wanasheria kutokuwa makini,"amesema Jafo.

Amewataka kuhakikisha wanasimamia vyema kesi za ardhi zinazowakabili wananchi wa chini ambao wengi wao hudhurumiwa na wenye uwezo na kusababisha malalamiko kwa wasimamizi wa sheria.

Mbali na hilo, pia Jafo amesema sheria nyingi za halmashauri zinatofautiana na maeneo husika ma kuwa na matatizo makubwa ya kimaandishi kutokana na kukinzana na sheria mama.

Amesema kutokana na sheria hizo kutoeleweka, inasababisha mikataba mingi ndani ya halmashauri hizo kutokuwa na umakini kwa kutoipendelea serikali na kuwapa kipaumbele walioingia mikataba hiyo, hali inayoonyesha kama hawapo wanasheria.