Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe. Anthon Mtaka akimkabidhi fedha Bw. Methesela Mrobi wakati wa zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III ,katika kijiji cha Mwamgoba, Wilaya ya Busega Mkoani humo.
Na Stella Kalinga
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amewataka viongozi wa kata na vijiji kuwabaini wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya TASAF III (PSSN) wanaojihusisha na ulevi na kuwaondoa katika orodha ya wanufaika wa mpango huo.
Mtaka ametoa agizo hilo wakati alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Mwamgoba wilayani Busega katika zoezi la uhawilishaji fedha za TASAF III PSSN, ambapo jumla ya shilingi 2,976,000 zimegawiwa kwa wanufaika 82 kijijini hapo.
Mtaka amesema lengo la mpango wa TASAF III ni kuwatoa watanzania katika hali ya umaskini kwa kuwapa ruzuku itakayowasadia kupata huduma muhimu ikiwa ni pamoja huduma za afya, kuwasaidia watoto wao waweze kwenda shule lakini baadhi ya wanufaika wamekuwa wakitumia fedha hizo kulewa badala ya kuanzisha miradi midogo midogo kama ufugaji wa kuku, mbuzi na kondoo pamoja na kilimo ili miradi hiyo iwasaidie kuwaongezea kipato.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu , Mhe. Anthon Mtaka akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Mwamgoba wilayani Busega (hawapo pichani) kabla ya zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku kwa wanufaika wa Mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III kijijini hapo, Wilayani Busega Mkoani humo.
"Hatuwezi kuleta fedha tukifikiri zitawasaidia kujikwamua katika Umaskini lakini mnashinda baa na vilabuni kulewa , wengine mnaongeza wake, tukiwabaini mtaondolewa kwenye huu mpango" , alisema Mtaka.