Ulikuwa usiku mujarabu kwa vijana wa Jurgen Klopp, Liverpool ndani ya dimba la Taifa la Ungereza,Wembley baada ya kuisambaratisha bila huruma bingwa wa Laliga Barcelona kwa mabao 4-0 na kuwaacha mashabiki wengi wa soka Ulimwenguni wasiamini walichokiona na kukisikia.
Wakicheza kwa kujituma huku wakifahamu wazi kuwa wanacheza na timu bora kabisa duniani, wachezaji wa Liverpool walihakikisha hawawapi nafasi wapinzani wao kumiliki mpira kwa kuingilia pasi zao,dakika ya 14, Lalana anamnyang'anya mpira Alex Vidal na kumpa pasi Firmino ambaye anamrudishia Lalana naye anampa tena Sadio Mane na bila ajizi anaukwamisha mpira huo wavuni,1-0.
Goli hilo linadumu hadi mapumziko, kipinndi cha pili kilipoanza inachukuwa dakika moja tu Liverpool wanaandika bao la pili kwa beki Mascherano kujifunga akiwa katika harakati za kuokoa mpira uliopigwa na Sadio Mane.
Dakika moja baadaye yaani dakika ya 47, Stewart anampokonya mpira Busquets na kumpenyezea pasi murua Diovick Origi anayewazidi mbio Gerard Pique na Mascherano nakupiga shuti linalopita katikati ya miguu (tobo) ya kipa wa Barcelona Terstegen. 3-0.
Katika kipindi hiki timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji zaidi ya 6 kwa kila timu, na hapo Barcelona walitawala zaidi mpira na kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Liverpool lakini ngome ya Liverpool ambayo iliongozwa na Lovren ilicheza kwa nidhamu ya hali ya juu na kufanikiwa kuzuia hatari zote.
Watu wakiamini kuwa mchezo unamalizika kwa hayo mabao matatu, Dakika ya 92 yaani dakika moja kabla ya mpira kumalizika kwa zile dakika za nyongeza Liverpool wanapora mpira katikati ya uwanja na kufanya shambulizi la kushitukiza, ambapo mpira wa krosi unapigwa na Markovic unatua kichwani kwa Grujic na kuupiga pembeni juu ya kona ya goli, waswahili hupenda kuita "anapotagia ndege" na mpira huo kutinga wavuni na kuandika bao la nne, hivyo kuhitimisha karamu hiyo ya mabao.4-0.