Friday, June 24, 2016

MAKOCHA WAPYA AZAM KUTUA MWISHO WA MWEZI.



MAKOCHA WAPYA AZAM KUTUA MWISHO WA MWEZI.
Na Zainab Nyamka,Globu ya Jamii.
MAKOCHA wapya wa timu ya Azam FC Zeben Hernandez pamoja na mtaalamu wa viungo, Jonas Garcia kutoka Hispania wanatarajiwa kutua mchini mwishoni mwa mwezi huu tayari kuanza maandalizi kuelekea msimu ujao wa ligi kuu. Makocha hao walisaini mikataba ya mwaka mmoja ya kuifundisha timu hiyo kuchukuwa nafasi ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo raia wa Uingereza, Stewart Hall aliyevunja mkataba wake na timu hiyo

Msemaji wa timu hiyo Jafar Iddy amesema walimu hao watakapowasili ndio mchakato wa usajili utakapoanza, kwa sasa uongozi wa timu hiyo hauwezi kusema kuwa unasajili ikiwa mwalimu atakuwa na mapendekezo yake na wao kama viongozi hawana utaalamu wowote katika mambo ya usajili bali kazi yao ni kuyafanyia kazi mapendekezo ya mwalimu kwa asilimia mia.

"Tutakaposema eti tunasajili tutakuwa tunadanganya umma kwani mwalimu atakapokuja atakuwa na mapendekezo yake na yeye ndiye anayefahamu mchezaji gani ni mzuri", amesema Jaffar. Kikubwa kitakachozingatiwa na timu hiyo ni kuhakikisha wachezaji wanaosajiliwa wanarekodi nzuri huku wakiwa msaada mkubwa kwa timu zao.

Amesema timu yao inatarajiwa kuingia kambini kuanzia Julai Mosi hivyo ni matumaini yao mwalimu ataweka wazi yupi anafaa na nani anapaswa kuondoka ndani ya kikosi hicho na licha ya kutoanza usajili lakini mategemeo yao ni kusaka wachezaji wenye uwezo kutoka Hispania pamoja na Afrika kwa ujumla.