Balozi wa Czech nchini Tanzania, mwenye makazi yake Nairobi nchini Kenya, Mhe. Pavel Rezac, ameishukuru serikali ya Tanzania kwa mapokezi mazuri aliyopewa Waziri wa Kilimo wa Czech, Mhe. Marian Jurecka, wakati wa ziara yake mapema mwezi huu wa Aprili, 2016.
Balozi Rezac amemwambia Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. John Haule, kuwa ziara ya Waziri Jurecka ilikuwa ya mafanikio makubwa, na kuwa nchi yake ina shauku ya kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa ya kukuza ushirikiano katika uwekezaji na biashara.
Amesema Czech iko tayari kushirikiana na Tanzania kujenga uwezo wa kuchakata bidhaa za kilimo na mifugo ili kuziongezea thamani kabla ya kuuzwa nje. Aidha, nchi hiyo ya Ulaya Mashariki inakusudia kubadilishana uzoefu na Tanzania katika tekinolojia ya viwanda, nishati na utengenezaji wa zana za kilimo.
Rasimu ya makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi hizi imewasilishwa kwa serikali ya Tanzania. Balozi Rezac amesema utekelezaji wa makubaliano hayo utaanza mara baada ya serikali ya Tanzania kuridhia.
Katika hatua nyingine, Balozi wa Ireland nchini Kenya, Mhe. Dkt. Vincent O'Neill, ameahidi kushawishi raia wa nchi yake wanaofanya biashara Kenya kuwekeza nchini Tanzania. Alitoa ahadi hiyo alipotembelea Ubalozi wa Tanzania Nairobi mwishoni mwa wiki iliyopita.
Balozi O'Neill amesema kuna uwezekano wa raia wa Ireland wanaoendesha biashara kwenye sekta za kilimo, benki na huduma nyingine za kifedha nchini Kenya kufungua matawi Tanzania.
Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. John Haule (kulia) akisalimiana na Balozi wa Ireland, Mhe. Dkt. Vincent O'Neill.
Balozi wa Czech nchini Tanzania mkaazi wa Nairobi, Mhe. Pavel Rezac (katikati), akizungumza na Balozi wa Tanzania Kenya, Mhe John Haule. Kushoto ni Mwambata wa Biashara na Uchumi wa Ubalozi wa Czech, Bwana Michal Mincev.