Mhe Waziri Ummy Mwalimu akibadilishana mawazo na washiriki wa majadiliano kuhusu ukeketaji.
Waziri Mwalimu akibadilishana mawazo na Waziri mwenzie Sicily Kariuki kutoka Kenya
Mhe. Waziri wa Afya.Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumzia uzefu wa Tanzania katika kukabiliana na tatizo la ukeketaji akiwa na wazungumzaji wengine katika Meza Kuu, kutoka kushoto ni Mke wa Rais wa Burkina Faso Bi. Sika Bella Kabore, Bw. Benoit Kalasi (UNFPA), Bi.Emma Bonino Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje Italia.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Mhe. Peter Serukamba akifuatilia majadiliano kuhusu tatizo la ukeketaji na adhari zake wa afya na maendeleo ya mtoto wa kike na mwanamke.
Wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi nao wakifuatilia majadiliano yaliyovutia washiriki wengi kuhusu madhara yatokanayo na ukeketaji na namna gani jamii inatakiwa kushirikiana kutokoza tatizo hilo.
Sehemu ya washiriki wa Mkutano na majadiliano kuhusu utokomezaji wa vitendo vya ukeketaji na uhusiano wake na utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu. Mkutano huu uliandaliwa kwa pamoja na Wakilishi za Kudumu za Tanzania, Burkina Faso, Italy, Iran, UNFPA na UNCEF.
Na Mwandishi Maalum, New York
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu ( Mb) amesisitiza kuwa ni kwa ushirikiano baina ya Serikali na jamii ndipo tatizo la ukeketaji kwa watoto wa kike na wanawake litakapoweza kutokomezwa.
Akaongeza kwamba, serikali inaweza kutunga sheria nyingi za kukabiliana na tatizo hilo lakini kama jamii yenyewe kuanzia ngazi ya familia isipotoa ushuriano wa dhani itachukua muda mrefu kwa tatizo hilo kutokomezwa. Alikuwa akizungumza wakati wa majadiliano ya mkutano wa kuhusu utokomezwaji vitendo vya ukeketaji kama sehemu muhimu ya utekelezaji wa Malengo Mapya ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030.
Waziri Ummy Mwalimu alikuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu katika mkutano huo uliowahusisha Mke wa Rais wa Burkina Faso, Bibi. Sika Bella Kabore, Mawaziri na Asasi za Kiraia na uliandaliwa kwa pamoja na Wakilishi za kudumu za Tanzania, Italy, Iran, Burkina Faso,UNFPA na UNICEF, ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa 60 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Wanawake.
Na kwa sababu hiyo, Waziri Ummy Mwalimu, amerejea kutoa wito kwa watanzania wote kwa katika ujumla wao wakiwamo wazee wa kimila, viongozi wa dini na vijana wakiume kutoa ushirikiano kwa serikali na wadau wengine ili hatimaye tatizo hilo ambalo linaelezwa kuwa siyo tu lina madhara makubwa kiafya na kisaikolojia lakini pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
"Tunatakiwa kufanya kazi kwa pamoja na katika umoja wetu, serikali peke yake haitaweza kulimaliza tatizo hili, ambalo imefikia mahali sasa wazazi kwa kuongopa mkono wa sharia wanaamua kuwafanyia ukeketeji watoto wa kike katika umri mdogo sana" Akaeleza Waziri.Akasema , Tanzania imebaini uelimishwaji na majadiliano yanayohusisha familia na vijana wakiume ni muhumu katika kuchangiza juhudi za serikali katika kukabili ukeketaji.
"Tunawaelimisha pia vijana wa kiume ili waelewe madhara ya ukeketaji kwa sababu wao ni wadau wakubwa kama waume watarajiwa. Lakini pia tunawaelimisha wasichana ambao wengine huamua kufanyiwa ukeketaji kwa hofu ya kutokuja olewa". Amesema Waziri.
Akasema Tanzania imeshukuru kwamba tatizo la Ukeketaji limepewa umuhimu na nafasi katika Ajenda mpya ya Maendeleo endelevu , ambapo katika lengo namba tano linalohusu Usawa wa Kijinsia, linaeleza zaidi umuhimu kumalizwa kwa vitendo vyote vibaya kama vile ndoa za utotoni, ndoa za kulazimishwa na ukeketaji ifikapo mwaka 2030.
Naye Mke wa Rais wa Burkina Faso, Bi. Sika Bella Kabore akizungumza katika mkutano huo amesema kuwa tatizo la ukeketaji ni la kimila na kitamaduni maeneo ambayo ameyataja kwamba yatanakiwa kufanyiwa kazi ya ziada ili kumaliza tatizo hilo.
"Tukiweza kulimaliza tatizo hilo tutakuwa pia tumefanikiwa katika kutetea haki za wanawake na watoto wa kike lakini pia tutamaliza ukatili dhidi ya wanawake, ukeketaji hauna nafasi katika Dini au Imani yoyote ile" Akasisiza Bi. Sika Bella Kabore.
Naye Dr. Lina Kilimo kutoka Kenya, yeye kwa upande wake amesema tatizo la ukeketaji si la Afrika au Asia peke yake bali ni la dunia nzima na kwamba kwa kuingizwa katika Agenda 2030 imedhihirisha wazi kwamba bila msukuko na ushirikiano kutoka pande zote itakuwa kazi kulimaliza tatizo hilo.
Kwa upande wake Dr. Morissanda Kouyate katika mchango wake amesema, ifikie mahali viongozi wasione aibu kulizungumzia hadharani tatizo na madhara ya ukeketaji na kwamba hakuna tena muda wa kusubiri. Madhumuni ya mkutano huu pamoja na mambo mengine yalikuwa ni kwa wajumbe wanaoudhuria mkutano wa 60 wa Kamisheni kuhusu hali ya Wanawake, kubadiliana uzoefu, changamoto pamoja na kujifunza mbinu ambazo nchi nyingine zinatumia kusukuma mbele jitihada za kutokomeza vitendo vya ukeketaji.
Inaelezwa kwamba Zaidi ya wanawake na watoto milioni 200 duniani kote wamefanyiwa ukeketaji , Afrika, Mashariki ya Kati, Asia, Latin America, Ulaya, Amerika ya Magharibi Australia na New Zeland. Kumalizwa kwa vitendo vya ukeketaji ni moja ya hatua muhimu katika kufanikisha malengo mengine ya maendeleo endelevu yakiwamo yanayohusu upatikanaji wa elimu bora, huduma za afya , ajira zenye hadhi na ukuaji wa uchumi