Tuesday, March 08, 2016

SAMAKI WALIOINGIZWA NCHINI KINYEMELA WATEKETEZWA



SAMAKI WALIOINGIZWA NCHINI KINYEMELA WATEKETEZWA

 Idara ya Uvuvi ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya ikishirikiana na kitengo cha usimamizi wa rasilimali ya uvuvi Kanda za Kuu Kusini, walikuwa katika ukaguzi maalumu dhidi ya wafanyabiashara ya samaki. Katika ukaguzi wao katika maduka yanayouza samaki wabichi iligundulika kwamba wengi wanauza samaki hao kinyume cha sheria na taratibu za uingizaji wa zao hilo.


Ni kutokana na hilo, zaidi ya kilo 844 za samaki wabichi aina ya magege (perege) zilizokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh 6,330,000 zilikamatwa katika maduka mbalimbali ya wauzaji hao na kisha kuteketezwa.
Kwa nini zilikamatwa?
Ni baada ya kugundulika kwmaba samaki hao waliingizwa nchini kinyemela kupitia njia za panya kutoka China na Zambia, kinyume na taratibu na sheria. Samaki hao walitiliwa mashaka kwa matumizi na afya ya binadamu kwa ujumla kutokana na kutokuwa na uthibitisho kutoka mamlaka husika ili kuona kama wanafaa kwa matumizi ya binadamu au la.
Ofisa Mfawidhi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi, Bakari Lulela, anasema samaki hao hufugwa katika mabwawa na mara nyingi huwa na kemikali ambazo ni sumu kwa mwili wa binadamu. Alisema ni kwa mantiki hiyo ni lazima wapitie kwa mkurugenzi wa uvuvi ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuwapima katika maabara ili kuthibitisha ubora wake na usalama, baada ya hapo mamlaka hutoa kibali cha kuuza.
Anasema samaki hao huwa wanaingizwa kwa njia ya panya hivyo hupoteza mapato ya serikali. Lulela amesisitiza kuwa ukaguzi huo waliofanya ni hifanyika pia kwa bidhaa zote nchini na kwamba husaidia kulinda afya ya binadamu "Hatufanyi ukaguzi kwa zao la samaki pekee bali na vyakula vingine ili kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salama," alisema.
Lulela anasena licha ya wafanyabiashara hao kuuza samaki wa aina tofauti wakiwemo sato, vibua, sangara na magege, aina ya magege ndio walioonekana wakiingizwa zaidi kiholela kupitia njia za panya. Kusambaa kwa samaki hao Baadhi ya maeneo yaliyobainika na wakazi wake kutumia samaki hao aina ya magege wanaohofiwa kuwa na suimu ni pamoja na Vwawa, Tunduma, Mbalizi, Mloho na Mbeya Mjini ambako kwa asilimia kubwa ndiyo maeneo yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa na tatizo hilo.
Mbali na uzoefu wa wafanyabiashara hao kufanya biashara ya samaki kwa muda usiopungua miaka 14, baadhi yao walishangazwa na hatua hiyo iliyochukuliwa dhidi yao kwani huuza samaki wa aina tofautitofauti bila ya kujua kama wana madhara kwa binadamu. Mpaka sasa Jeshi la Polisi linamshikilia Stella Chabuma, muuzaji wa samaki maeneo ya Kabwe. Kadhalika linawashikilia wafanyabisahara wa Iyunga, mjini Mbeya ambao hawakutajwa majina yao.
Ofisa Mfawidhi Idara ya Uvuvi Kituo cha Tunduma, Francis Mpatama ametoa onyo kwa wafanyabiashara wote wa Jiji la Mbeya hususan wanaofanya biashara ya chakula kuhakikisha wanafuata vtaratibu. "Serikali inajaribu kutoa onyo na angalizo kwa yeyote atakayebainika kufanya uhalifu wa aina yoyote ataweza kufilisiwa kabisa," alisisitiza. Pia aliwataka wafanyabiashara hao kuwa waangalifu na wajiridhishe sio tu waangalie samaki wana bei rahisi wanunue, ni lazima walinde afya ya mlaji.
Kwani kwa kufanya kinyume watakuwa wamevunja sheria ya uvuvi ya mwaka 2003 namba 22 na kanuni ya mwaka 2009 inayosema, kila samaki anayetoka nje ya nchi waingie na wapate kibali na wathibitishwe ubora wake ili walaji wasiathirike. Uteketezaji na utokomezaji wa bidhaa Mpatama alisisitiza kuwa mfanyabiashara yeyote atakayeratibu biashara zake bila kibali maalumu kutoka taasisi au mamlaka husika, bidhaa hiyo itateketezwa mara moja.
Aliongeza, kukiukwa kwa sheria hizo ndizo zilizosababisha halmashauri ya jiji kuteketeza samaki hao zaidi ya kilo 844 za samaki hao aina ya magege. Tamko kwa umma Adamu Mhagama kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa Mbeya anasema wananchi na wafanyabiashara hawajazuiwa kufanya biashara, bali wafuate taratibu zilizowekwa na mamlaka husika.
"Serikali haijawazuia wananchi na wafanyabiashara kwa ujumla kufanya biashara zao, bali wafuate mfumo ulio sahihi, utaratibu uko wazi kwa wavuvi wafuate taratibu zote zinazotakiwa, ili kulinda afya za wananchi," anasema Mhagama. Ofisa Uvuvi Jiji la Mbeya, Mary Malamula, ametoa onyo kwa wamiliki wote wa samaki aina ya magege kutoruhusiwa kufanya biashara hiyo hadi hapo mamlaka husika itakapofanya uchunguzi wa kina kuangalia na kuthibitisha kama samaki hao wanafaa kwa afya ya mlaji au la.
Meneja Mamlaka ya Chakula na Dawa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Karananga, anasema mwagizaji yeyote haruhusiwi kuingiza bidhaa nchini pasipo na kibali kutoka Taasisi ya Serikali au Mamlaka ya Chakula na Dawa. Anasema endapo anaingiza bidhaa yoyote inayohusu wanyama aende mamlaka ya chakula na dawa, hivyo hivyo na kwa upande wa mimea aende mamlaka za kilimo ili asajiliwe na kupata kibali ili kuhakikisha afya ya binadamu inalindwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa mkoa huo wameridhishwa na operesheni hiyo endelevu na wameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kuliangalia suala hilo kwa kina, kwani samaki ni sehemu ya mlo. Mkazi wa Iyunga, Amoni Mbilinyi, ameshukuru serikali kwa kuendelea kuwasaidia katika suala la afya ya binadamu ili wasidhurike na kuisihi iendelee kuchukua hatua kali dhidi ya wahalifu ili kujiepusha na kuingiza nchini bidha zisizo na ubora.
Naye mkazi mmoja wa Kabwe aliyefahamika kwa jina moja la mama Ndimbo alishangazwa na uingizwaji wa bidhaa za kimagendo kwani vyombo vya sheria vipo vilikuwa vinafanya nini hadi bidhaa hizo zisizo na ubaora kuingizwa nchini.
Hivyo ameiomba serikali iwaangalie kwa upya hao wanaopitisha hizo biashara kwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria, kwani wanaleta madhara makubwa kwa walaji. Operesheni hii ni endelevu katika Jiji la Mbeya kuhakikisha ubora wa chakula kwa afya ya mlaji kwa ujumla. Gloria Minga ni mchangiaji wa makala wa gazeti hili.