Thursday, March 17, 2016

MZEE JAJI WARIOBA AYASEMA HAYA JUU YA MAHAKAMA YA MAFISADI



MZEE JAJI WARIOBA AYASEMA HAYA JUU YA MAHAKAMA YA MAFISADI
Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesema ili mahakama maalum ya mafisadi ifanye kazi kwa ufanisi, inapaswa Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)  ziimarishwe.

Jaji Warioba alisema hayo jijini Dar es Salaam, baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, ofisini kwake.


Warioba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,  alisema suala la kuanzishwa kwa mahakama hiyo ni jambo zuri lakini kunahitajika vyombvo ambavyo vitafanya kazi na mahakama hiyo,  viimarishwe.

"Ni jambo zuri kuanzisha mahakama ya mafisadi, lakini chombo kimoja hakiwezi kushughulikia suala hili pekee yake. Kunahitajika  vyombo kama Polisi na Takukuru ambavyo vitafanya kazi na mahakama hii viimarishwe," alisema.

Warioba alisema kimsingi serikali ya awamu ya tano imeanza kazi vizuri katika kupambana na ufisadi na kufanikiwa kukusanya kodi, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kushirikiana na serikali ili kufanikisha kazi hiyo.

Naye Dk. Mwakyembe alisema wizara yake imejiwekea utaratibu wa kuwaalika viongozi wote waliowahi kuwa mawaziri katika wizara hiyo kufanya mazungumzo nao na kutoa ushauri wa kuboresha wizara hiyo.

Dk. Mwakyembe alisema mchakato wa kuanzisha mahakama ya mafisadi unaendelea na kwamba serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha tatizo la ufisadi linakomeshwa na watuhumiwa watashughulikiwa na mahakama hiyo.

Jaji Warioba, ambaye alikuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mwaka 1985 hadi 1990, aliwahi kuwa Waziri wa Sheria mwanzoni mwa miaka ya 1980. Pia aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katikati ya mika ya 1970 hadi 1985.