Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika wa Usuluhishi wa Mgogoro wa Libya amewasili jana jijini Tunis nchini Tunisia kushiriki Mkutano wa 8 wa Nchi Jirani ya Libya. Mkutano huo ulioitishwa na Serikali ya Tunisia ni muendelezo wa jitihada za nchi jirani kusaidia kuleta hali ya amani na usalama nchini Libya. Rais Mstaafy amewasili Tunis akitokea Salalah nchini Oman aliposhiriki katika Mkutano wa Kamati ya Bunge la Kuandika Katiba ya Libya.
Akiwa jijini Tunis, Rais Mstaafu Kikwete amefanya mazungumzo jana na Waziri wa Masuala ya Maghreb, Arab na Afrika wa Algeria Mheshimiwa Abdelkader Messaleh aliyemtembelea hotelini kwake. Katika mazungumzo yao, Waziri Messaleh alimpongeza Rais Mstaafu Kikwete kwa kuteuliwa na Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kusuluhisha mgogoro wa Libya. Alimuelezea hali ya usalama na kisisa ya Libya na mtizamo wa nchi yake juu ya namna bora ya utatuzi wa mgogoro huo.Alimhakikishia Rais Mstaafu ushirikiano wa Serikali ya Algeria katika jukumu lake alilokabidhiwa na Umoja wa Afrika.
Kwa upande wake, Rais Mstaafu Kikwete alimshukuru Waziri Abdelkader Messaleh kwa maelezo aliyompatia na ushirikiano aliomuahidi. Alimuelezea matumaini yake ya kupatikana kwa suluhu ya mgogoro huo madhali nchi jirani na Libya na Umoja wa Afrika zitashirikiana na wadau wote kuhakikisha mgogoro huo unatatulika. Alisisitiza kuwa hatimaye suluhu ya kudumu ya mgogoro wa Libya uko mikononi mwa wananchi wa Libya wenyewe.
Katika ziara yake nchini Tunisia, mbali na kuhudhuria Mkutano wa 8 wa Nchi Jirani na Libya, Rais Mstaafu Kikwete anatarajiwa pia kukutana na Waziri Mkuu Mteule na Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Libya (Presidency Council) Mheshimiwa Fayez Al-Sarraj, wadau wengine wa Libya pamoja na kutembelea Ofisi ya Ujumbe wa Umoja wa Afrika kwa Libya iliyoko jijini Tunis. Rais Mstaafu Jakaya Kikwete anatarajiwa kurejea nchini tarehe 25 Machi, 2016.
Mwakilishi Maalum wa AU wa Mgogoro wa Libya akizungumza na Waziri wa Masuala ya Maghreb, Arab na Afrika Mheshimiwa Abdelkader Messahel.
Mwakilishi Maalum wa AU wa mgogoro wa Libya akiagana na Waziri Abdelkadir Messahel wa Algeria baada ya mazungumzo yao.