Askofu wa Kanisa la God News for all Ministry, Dk. Charles Gadi, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhu kabla ya kuliombea taifa lipate mvua akiwa na wachungaji mbalimbali. Kulia ni Mchungaji Palemo Masawe.
Mchungaji Martini Ndaki (kushoto), akizungumza katika
mkutano huo.
Meza kuu kabla ya maombi.
Askofu Charles Gadi (wa tatu kutoka kushoto), akiongoza maombi ya kuliombea taifa lipate mvua. Kutoka kushoto ni Mchungaji Denis Komba, Mchungaji Martin Ndaki, Mchungaji Palemo Masawe, Mchungaji Denis Kumbilo, Mchungaji James Manyama na Mchungaji Leonard Kajuna.
Na Dotto Mwaibale
ASKOFU wa Kanisa la God News for all Ministry, Dk. Charles Gadi, ameliombea taifa lipate mvua kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa inayosababisha kuongezeka kwa joto nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo asubuhi, Askofu Gadi alisema, mabadiliko hayo ya kijiografia yamesababisha kukosekana kwa mvua za kutosha katika mwanzo wa masika wa mwezi wa tatu na kukithiri kwa joto kutokana na dunia kuwa karibu na jua(Equinox).
Alisema mvua za masika ni muhimu sana kwa kilimo, ufugaji, malisho ya wanyama mwitu wa nchini, mazao ya kudumu kama vile kahawa, migomba, michai na mito yote hayo yanategemea mvua za masika.
"Tukumbuke kuwa kuna kipindi kirefu hupita tangu mvua za masika hadi kukutana na za vuli ambapo ni karibu ya miezi mitano au sita pasipo na mvua, hivyo kama kukiwa na uhaba wa mvua za masika maana kipindi cha ukame kitaongezeka kwa miezi saba hadi miezi minane jambo ambalo ni hatari sana kwa kilimo na wanayama wetu.
"Joto la Equinox limekuwa kali kuliko wakati mwingine wowote ingawa lilitarajiwa kuchemsha maji ya bahari ili mvua ziwe nyingi lakini hali imekuwa kinyume, hivyo tunawaaasa watanzania wote bila kujali dini na itikadi ya mtu kuungana kwa pamoja kumuomba mungu ili ukame huu usiikumbe nchi yetu," alisema Askofu Gadi.
Alisema ni lazima kuomba ili ipatikane mvua za kutosha nan chi iweze kujitegemea kwa chakula ili fedha ambazo zingetumika kuagiza chakula nje ya nchi ziweze kutumika kwenye kuleta maendeleo ya kitaifa.
Aidha Askofu Gadi aliishukuru Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA)kwa kuendelea kutoa taarifa juu ya mabadiliko ya tabia nchi na kijiografia yanayosababisha kuongezeka kwa joto kwa kikwango kikubwa.
Askofu Gadi alifanya maombi hayo kwa kushirikiana na wachungaji wenzake ambao ni Mchungaji Denis Komba, Martin Ndaki, Palemo Masawe, Denis Kumbilo, James Manyama na Mchungaji Leonard Kajuna.