Wednesday, December 02, 2015

SERIKALI KUTUMIA TSH. BILIONI 5 KUHUDUMIA KAMBI ZA MADAKTARI BINGWA WA MOYO



SERIKALI KUTUMIA TSH. BILIONI 5 KUHUDUMIA KAMBI ZA MADAKTARI BINGWA WA MOYO
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 5 katika mwaka 2015/16 kwa ajili ya kuhudumia kambi za Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu ya magonjwa hayo kwa Watanzania.

Lengo la mkakati huo ni kuhakikisha Wagonjwa wengi wanahudumiwa katika kipindi kifupi pamoja na kupunguza gharama za kusafirisha wagonjwa nje ya nchi, ambao wengi wao husafiri kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya moyo, figo na saratani.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Donald Mmbando (Pichani)wakati wa ziara yake ya kutembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Dkt. Mbando alisema katika wiki ya kwanza iliyoanza wiki hii Madaktari hao wanatarajia kutoa huduma kwa wagonjwa 20 na kuifanya Serikali kuokoa kiasi cha Tsh. Milioni 500 ambazo zingetumika kuwasafirisha wagonjwa hao nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.

"Tumeokoa kiasi cha Tsh. Bilioni 1 zilizopaswa kutumika kuwapeleka nje ya nchi wagonjwa hawa, tutahakikisha kuwa Wataalamu hawa wanafanya kazi kwa pamoja na Madaktari wetu ili waweze kuwajengea uwezo katika kutibu magonjwa haya"  alisema Dkt. Mmando.

Alisema Serikali pia ipo katika mchakato wa kuzijengea uwezo hospitali mbalimbali nchini ikiwemo Taasisi ya Kansa ya Ocean Road na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kuziwezesha hospitali hizo kuwa na Wataalamu na majengo ya kisasa kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa Watanzania.

Aidha alisema Serikali imepanga kufanya mazungumzo na taasisi za kiraia na nyingine ikiwemo taasisi ya Rotary Club zilizokuwa zikisafarisha watoto wenye matatizo ya ugonjwa wa moyo, kuwekeza nguvu nchini kwani Tanzania kwa sasa ina wataalamu wa kutosha kwa ajili ya kuwatibu wagonja hao.

Kwa mujibu wa Mmbando alisema magonjwa ya moyo ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza, hivyo aliwataka Watanzania kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kuacha kunywa pombe na uvutaji wa sigara na kutazama desturi za ulaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Prof. Mohammed Janabi alisema katika kipindi cha wiki mbili ambazo madaktari hao watakuwepo hapa nchini wanaweza kuhudumia jumla ya wagonjwa 55, na hivyo kuifanya Serikali kuokoa kiasi cha Tsh. Bilioni 1.2