Matthew Rycroft, Mwakilishi wa Kudumu wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwa mwezi Novemba, akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani, mara baada ya Baraza Kuu la Usalama kumaliza kikao chake kilichojadili hali ya Burundi, kikao ambacho pia kilipitisha azimio ambalo pamoja na mambo mengine linamuunga mkono Rais wa Uganda Yoweri Museven ambaye aliteuliwa na Viongozi wenzie wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa msimamizi na mwezeshaji wa majadiliano kati ya pande zinazopinga nchini Burundi.
Na Mwandishi Maalum, New York
BARAZA Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali hali ya kuendelea kwa matukio ya mauaji, utesaji na vitendo vingine vya vinavyokiuka haki za binadamu nchini Burundi.
Pamoja na kukemea hali hiyo, Baraza Kuu la Usalama limeeleza kusudio la kuchukua hatua zaidi kwa nchi hiyo ya Burundi. Pamoja na kumwomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika kipindi cha siku kumi na tano awasilishe mbele ya Baraza hilo taarifa kuhusu uwepo wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi katika siku za baadaye.
Jana ( Alhamisi) Baraza hilo lilikutana katika kikao chake cha 7557 ajenda ilikuwa ni Burundi ambapo, Baraza kwa kauli moja lilipitisha Azimio namba 2248 (2015). Kupitia Azimio hilo, Baraza limetoa wito kwa pande zote nchini Burundi kujiepusha na kukataa fujo ikiwa ni pamoja na kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kutishia Amani na utulivu wa taifa hilo.
Vile Vile Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo kwa mwezi huu wa Novemba Rais wake ni Uingereza limekema vikali kauli za uchochezi zinazotolewa na baadhi ya watu ndani na nje ya Burundi, kauli ambazo kwa mujibu wa Baraza hilo zinalenga katika kushawishi chuki baina ya makundi ya watu nchini humo.
Kufuatia kauli hizo za uchochezi, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, limeitaka Serikali ya Burundi kuheshimu, kulinda na kuhakikisha haki za binadamu na misingi ya uhuru, kuheshimu utawala wa sheria pamoja na uwajibikaji wa uwazi dhidi ya fujo na itoe ushirikiano kwa Ofisi ya Kamisheni ya Haki za Binadamu.
Kupitia Azimio hilo Baraza Kuu pia limeitaka serikali ya Burundi kuwawajibisha wale wote watakaopatikana na hatia ya ukiukwaji ya Sheria ya Kimataifa ya haki za binadamu na unyanyasajji wa haki za binadamu.
Aidha kupitia Azimio hilo, Baraza Kuu la Usalama limetoa wito kwa Serikali ya Burundi kutoa ushirikiano katika majadiliano yanayoongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki na ambayo yameridhiwa na Umoja wa Afrika na limetaka kuitishwa haraka majadiliano yatakayokuwa jumuishi yakiwashirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Burundi ili kutafuta muafaka utakaokubaliwa na pande zote.
Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa pia kupitia Azimio hilo limesema linamuunga mkono kwa nguvu zote mwezeshaji wa majadiliano hayo ambaye ni Rais Yower Museveni wa Uganda aliyeteuliwa na Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika kusaidia mchakato wa majadiliano hayo, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa limemkaribisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupeleka timu ya wataalam ambao kwa kushirikiana na Serikali, Umoja wa Afrika na wadau wengine watabuni mbinu za kushughulikia matatizo ya kisiasa na kiusalama.