VIONGOZI wa dini ni watu wenye umuhimu mkubwa katika kila jamii. Ni viongozi ambao jukumu lao kubwa ni kuwaongoza waumini wao kiroho na kimwili. Kwa mwaka huu, viongozi hao hapa nchini wanatakiwa wasimame imara, kuwaongoza waumini wao, kuchagua viongozi waadilifu na wenye dhamira ya kweli ya uongozi.
Taifa linahitaji viongozi wazalendo, wachapakazi na waadilifu, watakaoweza kutatua matatizo na kero mbalimbali zilizopo nchini. Baadhi ya kero hizo ni ukosefu wa maji, barabara, zahanati na mawasiliano. Pia, kuna kero za rushwa na michango.
Tunawahimiza viongozi wa dini kuiombea nchi ipite salama katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu wa rais, wabunge, wawakilishi, madiwani na masheha. Tunasema hivyo kwa sababu uzoefu katika nchi nyingi za Afrika, unaonesha kwamba uchaguzi umekuwa ukitoa mwanya wa uvunjifu wa amani.
Hali hiyo haijawa hivyo hapa kwetu. Hata hivyo na sisi tunaweza kuwa kama nchi nyingine, iwapo yale yaliyozifikisha nchi huko ziliko leo hatutayaepuka. Mafanikio yetu ya kuendesha uchaguzi mkuu kwa amani na usalama, yametokana na tahadhari ambazo serikali na viongozi wa dini wamekuwa wakichukua.
Tuendelee kuchukua tahadhari hizo. Tusiwape mwanya wanasiasa wenye dhamira ovu ya kuwafarakanisha Watanzania. Tuendelee kukemea matumizi mabaya ya fedha, rushwa, hila, ghiliba na hujuma katika chaguzi.
Tuwakemee kwa nguvu zote wanasiasa wapenda madaraka, ambao wanatumia fedha kununua ushindi au kuendeleza ubaguzi wa rangi, kabila na dini. Viongozi wa dini na Watanzania hawapaswi kamwe kukaa kimya dhidi ya watu wanaokiuka maadili na kuchochea mifarakano nchini.
Hao si watu wema, watatufikisha pabaya. Hawaitakii mema nchi yetu. Kamwe tusiruhusu wachezee dini zetu, ambazo ni mhimili muhimu wa amani yetu. Ukabila unaweza kuhusisha eneo dogo, lakini dini huhusisha nchi nzima. Ukitokea mzozo wa dini, hakuna mtu, dini wala eneo litakalonusurika.
Tunatarajia viongozi wa dini hawatakuwa sehemu ya makundi ya wagombea au vyama vya siasa. Pia, hatutarajii viongozi wa dini watawapangia waumini wao vyama au viongozi wa kuwachagua katika uchaguzi wa mwaka huu. Tuna imani watawahimiza na kuwakumbusha waumini wao, kutumia haki na wajibu wao vizuri.
Aidha, tunaomba viongozi wa dini, kuongeza maradufu malezi ya jamii kimaadili hivi sasa ambapo nchi inakabiliwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili. Viongozi wa dini hawana budi kuwarudisha wanakondoo kwenye maadili mema na hilo linatokana na ukweli kuwa wanasikilizwa mno na waumini na pia watu wengi wanaofanya maasi na maovu ni waumini wao.