Na Sultani Kipingo wa Globu ya Jamii
Waziri wa Nchi(Kazi Maalum) Ofisi ya Rais Profesa Mark Mwandosya alikuwa Mgeni Rasmi katika kongamano lililoandaliwa kusherehekea Siku ya Taifa ya Bima, Ijumaa tarehe 25 Septemba 2015.
Kongamano hilo liliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Bima Tanzania (Insurance Institute of Tanzania - IIT) na Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania ( Tanzania Insurance Regulatory Authority-TIRA).
Kongamano hilo liliwakutanisha wadau wa sekta ya bima kutoka ndani na nje ya nchi, kutoka Wizara mbalimbali na taasisi za umma na sekta binafsi. Mada kuu ya kongamano hilo ilihusu Usimamizi wa Bima katika ili kuleta Maendeleo Endelevu.
Akihutubia Kongamano hilo Waziri Mwandosya amesisitiza umuhimu wa sekta ya Bima katika uchumi kama njia moja ya kuelekeza rasilimaili za taifa katika maeneo yanayoleta tija na faida, kuongeza akiba ya taifa na ya mwenye bima.
Amewataka wadau wa sekta ya bima wazingatie yafuatayo:
- kujenga uwezo wa rasilimali watu ili kukabiliana na mabadiliko makubwa katika uchumi na ongezeko la watu na mahitaji ya bima,
- kuifanya sekta ya bima ieleweke kwa wananchi kwa kuwa na mkakati wa uenezi na kutumia lugha nyepesi na inayoeleweka katika kuelezea dhana mbalimbali za bima,
- kutekeleza dhana ya " Bima katika Mstari wa Mbele" ili kuwafikia wananchi walio wengi waishio vijijini na maeneo ya miji wanakoishi wananchi wa kawaida,
- kuharakisha mfumo wa malipo ya bima, - kuwa na ufahamu wa maafa yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi na matukio asilia kama vile matetemeko ya ardhi, na mafuriko, kwa kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Hali ya Hewa, Idara ya Mazingira, Vyuo Vikuu , taasisi na wataalamu wengine katika masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa, mabadiliko ya majira na mabadiliko ya tabianchi. Kwani bima katika maeneo haya ni muhimu kwa taifa na jamii.
- kuangalia na kuishauri serikali kuhusu maeneo ya ziada ambayo ingefaa iwe lazima kisheria kuwa na bima, eneo kama vile bima za nyumba mijini dhidi ya moto.
- makampuni ya bima kufuatilia maendeleo utafiti, uchimbaji, usafrishaji na matumizi katika sekta ya mafuta na gesi.
- makampuni ya bima kuungana ili kushindana na makampuni ya nje katika kutoa bima katika zsekta muhimu na inayokua ya mafuta na gedi asilia.
Waziri wa Nchi(Kazi Maalum) Ofisi Profesa Mark Mwandosya akihutubia Kongamano lililoandaliwa kusherehekea Siku ya Taifa ya Bima, Ijumaa tarehe 25 Septemba 2015.
Washiriki wa kongamano hilo wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi(Kazi Maalum) Ofisi Profesa Mark Mwandosya
Waziri Mwandosya akitoa cheti kwa mmoja wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Sallam na Chuo cha Usimamizi wa Fedha waliofanya vizuri katika masoma ya yanayohusu Bima.
Waziri Mwandosya ,wa tano kushoto waliokaa akiwa na wanakongamano katika picha ya pamoja.