Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Dr John Magufuli akichaguliwa huenda nchi yetu ikashuhudia mapambano dhidi ya polisi na wananchi yakiongezeka kwa sababu serikali yake itaruhusu polisi kuuwa wananchi kwa kisingizio cha ujambazi.
Dr Magufuli katika kampeni zake kwenye uwanja wa Mashujaa mkoni Mtwara 02 Septemba 2015 alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa serikali yake haitamshitaki polisi yoyote atakayemuua jambazi mwenye silaha.
Dr Magufuli alikaririrwa akisema 'serikali yangu askari akipiga jambazi mwenye silaha kwa risasi hashtakiwi. Kila mara (majambazi) wanavamia vituo vya polisi, mbona hawavamii kambi za jeshi, jeshi la kujenga taifa au Ukonga FFU maana polisi wana nidhamu sasa wanawaonea na kuwaua'.
Wapiga kura wanajiuliza, kama kabla hajachaguliwa Dr Magufuli anaanza kuwaweka wananchi roho juu kiasi hiki, je akichaguliwa mapambano kati ya wananchi na vyombo vya dola yataongezeka kiasi gani?
Wananchi wanauliza swali hili kwa sababu ingawa hivi sasa hakuna polisi anayeruhusiwa kuhukumu watuhumiwa wa makosa mbali mbali ikiwa ni pamoja na watuhumiwa wa ujambazi, lakini umma umeshuhudia polisi wakiwauwa watu hovyo hovyo kwa tuhuma za ujambazi.
Wanauliza je Dr Magufuli akichaguliwa na polisi wakiruhusiwa rasmi kuwauwa watuhumiwa wa ujambazi—ni wananchi wangapi wasio na hatia watakaosukiwa zengwe la ujambazi na kuishia kuuwawa kikatili na polisi?
Hivi Magufuli ambaye amekuwa kiongozi wa serikali kwa zaidi ya mika 20 hajui kwamba polisi siyo mahakama na kwamba polisi haipaswi kutoa hukumu ya kifo kwa raia?
Wakati mgombea Dr Magufuli akitoa ahadi kwamba kwenye serikali yake polisi ndio watakaotoa hukumu ya kifo kwa watuhumiwa wa ujambazi; Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kuwa ni mahakama kuu ndiyo yenye mamlaha ya kutoa hukumu ya kifo.
Zaidi wananchi wanajiuliza, nchi itakuwa katika hatari kubwa kiasi gani Dr Magufuli akichaguliwa ambapo ataruhusu polisi kujichukulia sheria mkononi kuwauwa wananchi ambao pengine maisha magumu yametumbukiza kwenye ujambazi?
Lakini pia wananchi wanajiuliza je Dr Magufuli uchambuzi wake wa masuala ya kijamii umempa jibu kwamba polisi wakiwauwa ''majambazi wenye silaha'' ndio utakuwa mwisho wa mapambano kati ya wananchi na polisi?
Pengine Dr Magufuli anapaswa kujielimisha kujua kuwa chanzo cha ujambazi siyo wananchi na wala siyo polisi. Kadhalika chanzo cha mapambano katika ya polisi na wananchi siyo polisi wala wananchi
Dr Magufuli anapaswa mapambano kati ya polisi na wananchi wa ni kiashiria kimoja cha kuonyesha athari ya mfumo wa serikali ya CCM wa kutajirisha watawala na kufukarisha wananchi wengi.
Anapaswa kufahamu kwamba CCM baada ya kulitupa Azimiao la Arusha bila kuweka mbadala wake katika zama hizi mpya za utandawazi wizi ambapo mfumo wa uchumi unaotamba duniani baada ya ukomunisti kufa ni wa upebari ambao unaruhusu mtu uwezo wa kupata apate hata kama kwa wizi na wa kukosa afie mbali.
Matokeo yake sasa nchi yetu Tanzania ina kikundi kidogo cha watawala waliotajirika vya kutisha kwa kujigawia kibepari fedha za wananchi na mali za nchi (kutumia ujambazi wa kalamu na sheria) huku mamilioni ya wananchi wakiwepo polisi ambao hali zao za maisha ni mbaya wakitumia mbinu mbali mbali safi na chafu ukiwepo ujambazi ili maisha yaende.
Hali hii ni hatari kwa mustakabali wa amani ya nchi yetu. Lakini cha kushangaza ni kwamba Dr Magufuli hajui kwamba hata pale mamilioni ya wananchi walipotaka kuisaidia nchi kuondoa mfumo huu wa utawala unaozalisha makundi mengi ya kihalifu katika jamii—majambazi, panya road, wezi wa kutumia kalamu na sheria na kadhalika, CCM na serikali yake walikataa.
Wananchi walipendekeza Katiba Mpya CCM na serikali yake ikakataa kata kata na kuyazika maoni hayo pale Dodoma tena kwa mbwembwe na kutukana wananchi mwaka 2014.
Kiburi na jeuri ya watawala wa serikali ya CCM kukataa ushauri wa wananchi kutengeneza Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi ili kupunguza pengo la utajiri kati ya watawala na wananchi ndiyo sababu ya wananchi kuikataa CCM hata kama CCM itafanya propaganda na ufisadi kuonyesha inapendwa.
Tena wananchi wanajua kuwa Dr Magufuli akichaguliwa kuwa Rais maana yake ni kwamba serikali ya CCM kuendelea kuwa madarakani na hivyo ujambazi hautakwisha kwa kuuwa majambazi.
Badala yake amani ya nchi itawekwa rehani kwa sababu kwa polisi kuua majambazi—hasira ya wananchi itaongezeka siyo tu dhidi ya polisi bali dhidi ya kila chombo ambacho serikali itakitumia kudhibiti umma unaotamani madadiliko ya mfumo wa uongozi unaowafanya wananchi kuwa maskini na kudhalilishwa na vyombo vinavyopaswa kuwalinda raia.
Kwa hiyo vema CCM wakati huu wa kampeni isijidanganye, iwe ni kwa kutumia tafiti za kimkakati ama propaganda nyingine zozote kuwa wanakubalika kwa mamilioni ya wananchi wanaoteseka kwa umaskini na hivyo eti watashinda uchaguzi.
CCM na mgombea wao wa Urais Dr Magufuli wanapaswa kuwa na miwani itakayowaelekeza kuona kuwa kitendo cha wananchi wenye silaha (majambazi) kuvamia kituo cha polisi na kuuwa polisi, ni ishara tosha ya amani kutoweka nchini –maana ni mwanzo wa vita kati ya wananchi na polisi—kati ya wananchi na serikali yao.
Hii ni ishara tosha kwamba wananchi wameichoka serikali ya CCM iwe inaongozwa na Dr Magufuli au mwanamuziki maarufu nchini Diamond au mwana CCM yeyote mwingine atakayedhaniwa ni kivutio kwa wananchi.
Kadhalika CCM wanapaswa kufahamu kuwa kwa wananchi wengi kushabikia upinzani ni ishara nyingine tosha kwamba wananchi wameichoka CCM na serikali yake. Hivyo suluhisho siyo kuuwa upinzani, bali nchi kuweka mfumo mpya wa utawala ambao misingi yake wananchi wamependekeza kwenye Rasimu ya Katiba Mpya.
Kwa hiyo kama kweli CCM na serikali yake wanaitakia mema Tanzania yetu ---hasa amani ya kweli unaotokana na wananchi wengi kuridhika na maisha badala ya viongozi peke yake kuwa matajiri wa kukufuru, ni vema na ni muhimu sana wakaheshimu maamuzi ya wananchi watakayoyafanya kupitia sanduku huru la kura hapo tarehe 25 Oktoba mwaka huu 2015. Mungu ibariki Tanzania.
Note: Ninaruhusu yeyote mwenye kutaka kuisambaza, kuichapisha Makala hii afanye hivyo. Lengo sote tushiriki kuijenga Tanzania yetu.
Ananilea Nkya
E-mail: ananilea_nkya@yahoo.com