Tuesday, August 11, 2015

LOWASSA Awa Kivutio Kwa Vijana......Wajitokeza Barabarani na 'MAJENEZA' Wakimtaka Magufuli Naye Ahamie UKAWA


LOWASSA Awa Kivutio Kwa Vijana......Wajitokeza Barabarani na 'MAJENEZA' Wakimtaka Magufuli Naye Ahamie UKAWA

MAKUNDI ya vijana jana yalionekana kumiminika mithili ya kumbikumbi warukapo wakati wa masika wakimsindikiza mgombea urais Edward Lowassa anayewakilisha Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Lowassa ambaye alifika makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu za kugombea, alifanya hivyo chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ulioanzishwa wakati wa Bunge Maalum la Katiba.

Makundi ya vijana yalionekana katika nyuso zilizojaa furaha na bashasha wakithibitisha imani yao kwa Lowassa ambaye alihamia Chadema baada ya kukatwa jina lake katika kile alichokieleza mwenyewe "mpango wa kunihujumu."

Vijana walijitokeza na masanduku ya mfano wa jeneza, wakiimba nyimbo za kumtaka Dk. John Magufuli anayegombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ahame chama hicho na kuingia kambi ya Ukawa.

Vijana wanaonekana kuguswa na nguvu iliyoimarika katika kundi la UKAWA wakiamini nguvu hiyo itakidhi kiu yao ya mabadiliko ya uongozi nchini.

Lowassa alihama CCM mapema mwezi huu na kujiunga Chadema, chama alichosema kimepata mafanikio makubwa katika kujenga mtandao nchi nzima.

Tangu alipohama CCM, Lowassa amekuwa akirudia maneno yaliyosemwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwamba"Watanzania wanataka mabadiliko na wakiyakosa ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM," akimaanisha kuwa ameingia Chadema na kubeba dhamana ya UKAWA ili kusaidiana na viongozi wao kutafuta mabadiliko waliyoshindwa kuyaleta CCM.

Hali imekuwa tofauti na ilivyotarajiwa kuwa kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, kuwa kungesababisha mpasuko CUF na UKAWA, badala yake maelfu ya wanachama wanaendelea kumuunga mkono Lowassa kuwa Rais.

"Nimepata faraja sana kujiunga na Ukawa japo kumekuwa na misukosuko. Ni lazima tuwe wamoja, mtunze kadi zenu za kupigia kura. Mwaka huu lazima tushinde, tena kwa kura asilimia 90 ili wakiiba asilimia 10 tusisikitike," alisema Lowassa alipozuru Ofisi Kuu za CUF juzi ambako pia alihutubia Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lililofanya kikao cha dharura kutafuta kuziba nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa chama hicho.

Lowassa aliondoa uvumi kwamba akichaguliwa kutakuwa na vurugu nchini. Alisema kutakuwa na utulivu mkubwa na wafanyabiashara hawana sababu ya kuhofu.