Sunday, May 17, 2015

NYALANDU NA MKUU WA WILAYA karagwe walipuliwa bungeni baada ya kujimilikisha ardhi kifisadi



NYALANDU NA MKUU WA WILAYA karagwe walipuliwa bungeni baada ya kujimilikisha ardhi kifisadi
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.

Viongozi wawili wa serikali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Mkuu wa Wilaya  (DC) ya Karagwe mkoani Kagera, Deny Rwegasira, wamelipuliwa bungeni wakihusishwa na kuchochea migogoro ya ardhi.

Nyalandu alishitakiwa bungeni kuwa amejimilikisha kinyemela shamba la wanavijiji mkoani Tanga lenye ekari 500 analowakodisha wajane Shilingi 250,000 wanapolilima.

Madai hayo ni kwa mujibu wa Mbunge wa Viti Maalum, Rebecca Mngodo (Chadema),  aliyoyatoa bungeni jana.

DC wa Karagwe naye anaelezwa kuwa anawapora wakulima na wafugaji ardhi wa kijiji hicho cha mpakani na kuwamilikisha wafugaji wa Wanyaruanda.

NYALANDU

Akichangia hotuba ya Waziri Mkuu, Mngodo alisema Aprili  25, 2014 , Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alifuta hati za usajili za mashamba pori la mkonge mkoani Tanga likiwamo la pori la Kikuletwa.

Kwa utaratibu huo shamba hilo lililokuwa ligawanywe kwa wananchi, lakini halikugawanywa hivyo akalazimika kuwasiliana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu ucheleweshaji wa mchakato huo uliokuwa unawanyima wanavijiji ardhi.

"Nilipomweleza aliwasiliana na watendaji ili shamba hilo lirudishwe mikononi mwa wananchi. Niliamini kuwa hilo limefanyika,  lakini haikuwa hivyo. Kutokana na CCM kujenga matabaka ya maskini na matajiri, shamba hilo limechukuliwa na baadhi ya watu akiwamo Nyalandu anayemilika eka 500 anazowakodisha wanawake wajane. "

Aliongeza kuwa hadi sasa hakuna utatuzi na wananchi wanaendelea kuwa maskini wakati viongozi wa CCM wanazidi kuwa matabaka ya wenye nacho.

DC KARAGWE  

Rwegasira alishitakiwa kwa  Ofisi ya Waziri Mkuu na mbunge wa Karagwe (CCM) Gosbert Blandes, kuwa anawafukuza wanavijiji na wapiga kura wake wa Kanogo wilayani humo, akiwataka waachie ardhi yao kuwapisha wahamiaji haramu kutoka Rwanda.

Alisema wakazi hao wanaoishi mpakani na Rwanda wanafukuzwa ili Wanyaruanda wapate eneo la kulisha mifugo.

Alimponda Rwegasira kuwa yuko kimwili Tanzania lakini  kiroho na kiakili yuko Rwanda na kutaka ofisi hiyo iwaondolee mkuu huyo wa wilaya aliyechoka.

Alieleza kuwa DC aliwatuma polisi na bunduki kwenda kuwahamisha wananchi lakini kama mbunge aliwataka wanavijiji wapambane naye kikamilifu.

Blandes alituhumiwa kuwa licha ya kutumia madaraka yake vibaya na kukamata viongozi wenzake na kuwaweka ndani hajamkamata kwa vile anamuogopa mbunge huyo.

Alilitangazia Bunge kuwa iwapo serikali haitamuondoa , yeye na wananchi watapambana naye na siku moja watafanya jambo ambalo litashangaza taifa.

KIRIGINI AMBANA BLANDES

Mkuu wa Wilaya ya Maswa,  Rose Kirigini, ambaye pia ni mbunge wa CCM (Viti) Maalum, aliomba muongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, kuhusu tuhuma za Rwegasira.

Akizungumza bungeni alitaka kujua maelezo ya serikali kuhusu kauli ya mbunge huyo dhidi ya DC wa Karagwe.

"Mbunge wa Karagwe, ametoa lugha za vitisho na uchochezi dhidi ya Mkuu wa Wilaya ambaye hata sasa yuko hapa bungeni. DC  ndiye mwakilishi wa mheshimiwa Rais na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya." Alisema na kutaka kauli ya serikali.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Jennister Mhagama, alisema maelezo ya mbunge yamechukuliwa na serikali italifanyia kazi suala hilo.

Aliongeza kuwa hatua zitafuata kwa kuzingatia misingi na taratibu za kisheria za utumishi wa umma. 

Chanzo :nipashe