Bariadi. Polisi mkoani Simiyu inamshikilia mkazi wa Kijiji cha Bukigi, Kata ya Malampaka wilayani Maswa, kwa tuhuma za kukutwa na viungo vinavyosadikiwa kuwa ni vya binadamu likiwamo fuvu la kichwa.
Mtuhumiwa huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa kijiji hicho na mganga wa kienyeji, alikamatwa nyumbani kwake baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa alikuwa amewahifadhi majambazi ili awazindike.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Gemini Mushi alisema jana kuwa mwenyekiti huyo alikamatwa Mei 9, kijijini hapo baada ya kupata taarifa ya kuwapo majambazi nyumbani kwa mwenyekiti huyo. Alisema baada ya taarifa hizo, polisi walifanya msako nyumbani kwa mwenyekiti huyo na kufanikiwa kukamata vitu hivyo.
Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kama viungo hivyo ni vya binadamu na kama anahusika navyo, kwa sababu vilikutwa nje ya nyumba yake.