Raia 12 wa Iran na Pakistan wanaokabiliwa na kesi ya kukutwa na kuingiza nchini dawa za kulevya aina ya heroin kilo 200.5, zenye thamani ya sh. bilioni 9.02, wamelalamikia kucheleweshwa kwa kesi yao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Washtakiwa hao ni Kapteni Ayoub Mohamed, Buksh Mohamed, Fahiz Dauda, Khalid Ally, Abdul Somad, Saeed Sahury, Bashir Afraz, Morad Gwaram na Hazir Azad, wote raia wa Iran ambao walikamatwa kwenye Bahari ya Tanzania.
Wengine ni Buksh Mohamed, Rahim Baksh na Abdul Bakashi kutoka Pakistan ambao wote ni wavuvi.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda, Wakili wa Serikali Janeth Kitali, alidai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa.
Baada ya maelezo hayo, mshtakiwa wa kwanza Ayoub ambaye alikuwa nahodha wa meli iliyokutwa na shehena ya dawa hizo, alidai bora wapigwe risasi wafe kuliko kucheleweshewa hukumu yao.
Alisema kila wanapofikishwa mahakamani hapo, wanaambiwa upelelezi haujakamilika na muda unakwenda wakizidi kuteseka gerezani ambako mazingira yake si mazuri.
Hata hivyo, Hakimu Kaluyenda aliahirisha shauri hilo hadi Mei 5, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa hao walirudishwa rumande.
Inadaiwa Februari 4, 2014, washtakiwa hao walikamatwa na dawa za kulevya aina ya heroin kilo 200.5, zikiwa na thamani ya sh. bilioni 9.2, wakizisafirisha kwa njia ya bahari.